UNICEF NA TET KUENDELEA KUSHIRIKIANA KATIKA KUBORESHA ELIMU NCHINI


::::::::::

 Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la kulinda na kutetea haki za watoto (UNICEF) kuendelea kushirikiana katika kuboresha Sekta ya Elimu nchini hasa katika eneo la mafunzo endelevu kwa walimu kazini (MEWAKA) na maktaba mtandao. 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt. Aneth Komba leo Agosti 7, 2025 alipopokea ugeni kutoka UNICEF ulioongozwa na Simone Vis katika ziara fupi ya kujifunza maboresho ya Mtaala na matumizi ya teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji iliyofanyika katika taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam. 

“TET na UNICEF kwa pomoja tumeshirikiana katika eneo la utekelezaji wa maboresho ya mitaala yaliyofanyika hususani katika utoaji wa mafunzo endelevu kwa walimu kazini na katika eneo la kuandaa maktaba mtandao.“ Amesema Dkt. Komba.

 Kwa upande wake Msimamizi wa masuala ya elimu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF ) nchini Tanzania  Simone Vis amesema, UNICEF itaendelea kutoa ushirikiano kwa TET katika maboresho ya Elimu ikiwemo maendeleo ya walimu hasa waliopo vijijini kutokana na hali ya mazingira yao yalivyo ili walimu waweze kufanya kazi yao kwa ufanisi.

 Ujumbe huo wa UNICEF ukiambatana na baadhi ya wajumbe wa menejimenti ya TET umepata wasaa wa kutembelea na kujionea teknolojia zinatumika TET katika kufundishia na kujifunzia ikiwemo darasa janja, maabara ya kompyuta, studio ya televisheni na studio ya sauti.