Conte, Casemiro wafunika Yanga | Mwanaspoti

KATIKA kambi ya mazoezi ya Yanga yanayoendelea kwa sasa pale KMC Complex, Dar es Salaam ikijiandaa na msimu mpya wa mashindano kuna balaa la mastaa wapya wa timu hiyo ambao Mwanaspoti lilipata nafasi ya kuwaona wanakiwasha, lakini gumzo ni Moussa Bala Conte na AbdulNasir Mohammed ‘Casemiro’.

Yanga inajifua karibu wiki sasa kwenye uwanja huo uliopo eneo la Mwenge ambapo Mwanaspoti limefanikiwa kupata nafasi ya kuyatazama mazoezi hayo na kwamba kivutio kikubwa ni mastaa wapya wa timu hiyo lakini kinara ni Conte ambaye akiwa katikati ya uwanja kuna kazi ya maana ameanza kuitambulisha.

Conte aliyesajiliwa na Yanga akitokea CS Sfaxien ya Tunisia baada ya mabingwa hao wa soka Tanzania kuununua mkataba wake, anaonyesha shoo nzuri kwa ubora wa kupiga pasi tofauti lakini pia kukaba.

Tuanze na pasi zake ni kwamba jamaa anajua kupiga pasi ndefu ambapo anapokea na kushoto kisha kuitupa na kulia na ukimpa na kulia anaitupa ndefu kwa mguu wa kushoto.

Kiungo huyo raia wa Guinea amekuwa hodari kwa kupiga pasi fupi na ndefu ambapo kwa mazoezi ya jana alitumia dakika 40 kupiga pasi 38 na ndani ya hizo ikapotea moja tu ambayo winga mpya wa timu hiyo Ofen Chikola aliichelewa kuinasa.

Ubora wake mwingine ni katika eneo la kukaba ambapo kuna dakika anakichafua kwa kukaba kwa nguvu kisha wakati mwingine akikaba kwa kufunga njia akizinasa zile pasi za hesabu ndefu.

Conte akiwa mazoezini anaonyesha uchangamfu mkubwa akicheka na wenzake na kuwaelekeza, huku akizidi kuzoezna na wenzake.

Achana na Conte kuna yule Abdulnassir Mohammed ‘Casemiro’ aliyesajiliwa kutoka visiwani Zanzibar, naye ana ‘kijiji’ chake kwa ubora wake wa kukaba kwa nguvu.

Casemiro, ametumwa kukaba tu na akishaikamata mali basi anapambana kusogeza mashambulizi mbele akiwavutia wengi kutokana na kazi anayoifanya.

Kuna Mohamed Doumbia katika mazoezi hayo ameonyesha sio kiungo rahisi kupoteza mpira ukiwa kwenye miguu yake lakini ubora zaidi ni namna anavyojua kupiga pasi za haraka za kwenda mbele huku akianza kupiga mashuti taratibu.

Yanga inaendelea na mazoezi kujiandaa na msimu mpya, ikiwa chini ya kocha mpya Romain Folz, ambapo ndani ya siku chache kutoka sasa kikosi hicho kitaondoka nchini kwenda Rwanda kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Rayon Sports kwa mwaliko maalum.

Katika hatua nyingine, klabu ya Yanga jana ililamba dili nono likiongeza mkataba na kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya Haier wa miaka mitatu wenye thamani ya Sh3.3 bilioni.

Wadhamini hao sasa watakuwa kwenye jezi za timu hiyo mkono wa kushoto ikiwa ni mkataba wa kwanza kwa msimu ujao, huku wadhamini wakuu SportPesa wakitarajiwa kuongeza mkataba mwingine hivi karibuni baada ya ule wa awali wa miaka mitatu uliokuwa na thamani ya Sh 12.3 kuisha.