Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wameonya kuwa si kila muwasho wa sehemu za siri unatokana na maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), magonjwa ya mfumo wa uzazi (PID) au fangasi, bali pia huweza kuwa ishara ya ugonjwa wa ngozi ujulikanao kama lichen sclerosus, ambao huathiri zaidi wanawake waliokoma hedhi, lakini pia huwapata watoto na watu wa jinsi zote.
Ugonjwa huu wa ngozi unaosababisha uchochezi wa muda mrefu, huathiri zaidi maeneo ya siri ya wanawake na wanaume pamoja na sehemu ya haja kubwa. Licha ya kuwa nadra, ugonjwa huu huweza kuambatana na madhara makubwa ikiwa hautagunduliwa na kutibiwa mapema.
Mara nyingi athari zake hutokea sehemu za mwili zisizoota nywele kama tumboni lakini shida kubwa hasa hutokea sehemu za siri za binadamu. Kwa mwanamke hutokea katikati ya mashavu ya uke na sehemu ya haja kubwa, ilhali kwa mwanaume huathiri kwenye ngozi laini ya kichwa cha uume, na sehemu ya njia ya mkojo.
Amina Rajabu si jina lake halisi, ni mmoja wa waathirika wa ugonjwa huu. Akizungumza na Mwananchi, anasema alianza kuhisi muwasho mkali ukeni uliomsababishia kukosa amani mbele za watu.
“Nilikuwa najikuna hadi nakosa raha. Rafiki yangu alinieleza kuwa ni fangasi akanishauri nitumie dawa za Fluconazole. Nilipozitumia muwasho ulipungua kwa muda, lakini baadaye hali ilizidi kuwa mbaya zaidi,” anasema.
Anaongeza kuwa alianza kuona majimaji yenye harufu kutoka ukeni, rangi ya ngozi ilibadilika kuwa nyekundu na kujaa malengelenge. Akidhani ni ugonjwa wa zinaa, aliogopa kwenda hospitali hadi alipopata homa na kulazimika kutembelea zahanati.
“Nilipoenda hospitali niliambiwa ni UTI kali, nikapewa antibiotics na dawa za kupaka, lakini hali haikubadilika. Baadaye nilipewa rufaa Muhimbili ambako nilikutana na daktari bingwa aliyenisaidia kujua chanzo cha tatizo. Sasa naendelea vizuri,” anasema.
Kwa upande mwingine, mwanamama aitwaye Meenakshi anasema alikaa na dalili kwa zaidi ya miaka 10 bila kueleza kwa kile alichokisema kuona aibu. Baada ya madaktari 13 kumfanyia uchunguzi kwa miaka mingine 12, hatimaye aligundulika kuwa na lichen sclerosus na kupata tiba.
“Nilipata nguvu mpya. Nina maisha mapya sasa. Usiogope kuzungumza,” alisema.
Clare, mwanamke mwingine aliyeteseka kwa karibu miaka 40, alianza kwa muwasho, malengelenge na maumivu. Alipimwa mara kadhaa na kuambiwa ni fangasi, hadi alipopata utambuzi sahihi wa ugonjwa huo. Hata hivyo, kuchelewa kwa matibabu kulimpelekea kupata saratani ya sehemu za siri na kulazimika kufanyiwa upasuaji mara kadhaa. Anaendelea na matibabu hadi sasa.
Akizungumza na Mwananchi, Daktari bingwa wa magonjwa ya ngozi na ya kujamiana, Dk Ramadhani Jitihadi, anasema ugonjwa huu hausababishwi kwa njia za kujamiiana, kugusana wala uchafu wa sehemu za siri bali huwapata zaidi watu wenye upungufu wa kinga mwilini, lakini unahusishwa na mchanganyiko wa urithi wa vinasaba na uharibifu au muwasho wa ngozi. Kwenye familia mama anaweza kuwa nao akamrithisha mtoto wake.
“Unajua dalili za ugonjwa huu inategemea umeathiri sana upande gani, maana kuna sehemu ya ndani za siri (uke na uume) na sehemu ya nje (tumboni). Lakini dalili za awali sehemu ya ngozi iliyoathirika inakuwa nyekundu, kuwasha sana, malengelenge, ngozi kuwa ngumu na kubanduka magamba kutokana na kujikuna sana ambapo husababisha mabaka meupe kwenye sehemu za siri, makovu yanayopelekea maumivu makali kutokana na kuziba sehemu ya njia ya mkojo,”anaeleza.
Anasema dalili hizi kwa wanaume hutokea sehemu ya ngozi laini ya juu ya uume, ambapo kutokana na muwasho anaoupata mwathirika sehemu hiyo huanza kubadilika rangi kuwa nyekundu, kuwasha, ngozi kuwa ngumu na kutoa mabaka meupe ambayo husababisha kovu litakalobana sehemu ya njia ya mkojo na mgonjwa kupata maumivu makali wakati wa kukojoa au wakati wa kujamiana akiwa anatoa mbegu za uzazi. Wakati mwingine hutoa damu wakati wa kujisaidia haja ndogo.
“Wagonjwa wengi wanapokuja hospitali wakiona dalili hizo, hudhani wana UTI au maambukizi ya magonjwa ya ngono, mara nyingi wanaenda kwa madaktari wa mkojo kupima, shida inakuwa mpaka ugundulike unashida gani itategemea na atakayekupima. Watu wengi hawana utaratibu wa kwenda moja kwa moja kwa madaktari bingwa, mtu anaanzia vituo vya afya huko hujitibia mpaka tatizo lijulikane inakuwa lishakuwa kubwa,”anasema.
Anasema wanawake wao ndio waathirika wakubwa wa huu ugonjwa maana huwashambulia zaidi sehemu za siri za uke katikati ya mashavu ya ukeni kusababisha muwasho, alama za ngozi nyeupe au mabaka, na mara nyingi hufanya ngozi kuwa nyembamba au yenye mikunjo sehemu za siri.
Wakati mwingine husababisha malengelenge, kutokwa na majimaji yenye harufu kali ambayo husababisha bakteria ambao hutazalisha fangasi ya sehemu za uke inayoitwa candida. Madhara haya yatasambaa mpaka sehemu ya haja kubwa na kusababisha maumivu makali wakati wa kujisaidia.
“Zaidi ya asilimia 90 ugonjwa huu huathiri sehemu za siri, na asilimia 10 ni sehemu ya nje ya ngozi kama tumboni, lakini eneo hili hutokea mara chache sana. Wanawake ni zaidi ya asilimia 90 wanapata ugonjwa huu kuliko wanaume, kutokana na wanawake wengi kuwa na shida ya ‘hormone imbalance’ au ukomo wa hedhi.”anasema.
Daktari wa watoto katika Hospitali ya Dar Group, Groriamalia Kunambi anasema changamoto kubwa ya ugonjwa huu ni ukosefu wa uelewa.
Hili tatizo lipo kiasi chake nchini na duniani shida huwezi kujua lipo kwa ukubwa wa kiasi gani kutokana na wagonjwa wengi hawana uelewa na wanachoumwa na ndio maana mara nyingi hukimbilia kutibu kile kinachomsumbua kwa wakati huo, kama ni muwasho basi atatafuta dawa za fangasi. Mimi nimeshakutana na kesi kama hizi kama sita lakini ni muda kidogo,” anasema.
Anaongeza: “Kabla sijawa daktari wa watoto nilikuwa daktari wa magonjwa ya binadamu kiujumla katika hospitali mbalimbali ambazo nilishawahi kufanya nazo kazi. Nilishawahi kukutana na wagonjwa wa tatizo hilo, mgonjwa akikuelezea tatizo lake yeye huhisi ni fangasi ya kawaida. Ukimwambia sasa nionyeshe tuone hali ilivyo unagundua hii ni lichen, kinachofanyika ni kumwelekeza dawa za kutumia lakini kwa uchunguzi zaidi unamshauri akaonane na daktari bingwa wa magonjwa ya ngozi ili kupata tiba zaidi.
“Ugonjwa huu dalili zake unafanana na candida (fangasi ukeni) tofauti yake huu hauingia ndani kabisa kuweza kuathiri via vya uzazi.Wenyewe unashambulia ngozi ya nje ya uke, kichwa cha uume na sehemu ya haja kubwa,” anasema.
Dalili kubwa ni muwasho sehemu za siri, maumivu, hisia ya kuungua, na maumivu wakati wa kujamiiana. Ngozi huwa ngumu, huvimba na kutoa magamba kutokana na kujikuna. Mgonjwa huweza kupata malengelenge na vidonda.
Ikiwa haitatibiwa mapema, ugonjwa huu huweza kusababisha kovu linaloathiri kukojoa, kujamiiana, au kutoa haja kubwa. Aidha, huongeza hatari ya kupata saratani aina ya squamous cell carcinoma ya ngozi ya sehemu za siri. Takribani asilimia tano ya waathirika wa lichen sclerosus huweza kupata saratani hiyo endapo hawatapata tiba mapema.
‘’Nashauri uonapo dalili hizi kimbilia hospitali kubwa kaonane na daktari bingwa wa ugonjwa husika ili uanze tiba mapema, kusema kuuepuka ni ngumu kwa sababu hauambukizi kama magonjwa mengine. Kitakachofanyika baada ya vipimo utapata dawa za kupaka zenye steroid wakati mwingine huwa tunawachoma sindano ili kupunguza tatizo. Matibabu yake ni ya muda mrefu hivyo mgonjwa anapaswa kuhudhuria kliniki kila baada ya muda fulani, unaweza kuwa mwezi au wiki mbili ili kuangalia maendeleo ya tatizo alilonalo,” anasema Dk Jitihadi.
Ingawa hakuna tiba ya moja kwa moja, matibabu kwa kutumia steroid (dawa za ngozi zinazozuia mfumo wa kinga mwilini kushambuliwa) inaweza kusaidia kudhibiti dalili na kuzuia matatizo.
Dk Jitihadi anashauri wagonjwa kuwahi hospitali kubwa na kuonana na daktari bingwa wa ngozi pindi wanapoona dalili hizo. Matibabu hutumia dawa za steroid kama clobetasol propionate kupunguza uvimbe na muwasho. Wakati mwingine sindano huweza kutolewa.
“Hakuna tiba ya moja kwa moja, lakini dalili zinaweza kudhibitiwa. Wagonjwa wanapaswa kuhudhuria kliniki mara kwa mara ili kufuatilia maendeleo ya matibabu. Ugonjwa huu unahitaji uangalizi wa muda mrefu,” anabainisha.