Wakulima 5,000 wajisajili kwenye mfumo kupata mbolea

Dodoma. Jumla ya wakulima 5,156 wamejisajili kwenye mfumo wa kusajili wakulima nchini ili waweze kupata ruzuku ya mbolea kutoka Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (Tosci) kwenye maonyesho ya wakulima, wavuvi na wafugaji (Nanenane) jijini Dodoma.

‎Aidha, wakulima hao wamepata elimu ya kujua mbegu bora zilizothibitishwa na Tosci ili kuondokana na malalamiko ya kununua mbegu zisizokuwa na ubora kutoka kwa wasambazaji ambao hawajathibitishwa.

‎Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Agosti 8, 2025 kwenye maonyesho ya Nanenane jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Tosci, Nyasebwa Chimagu amesema maonyesho hayo yametumika kama darasa kwa wakulima kujua mbegu bora na bandia.

‎Amesema kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wakulima kuuziwa mbegu bandia ambazo hazioti au kutoa mazao wasiyoyatarajia.

‎Amesema kupitia maonyesho hayo wakulima wamepata nafasi ya kutambua mbegu bora zilizothibitishwa na Tosci kwa kutumia alama maalumu iliyopo kwenye kifungashio ambayo inaonyesha kama mbegu hiyo ni bora au laa.

“Kwa siku hizi nane tumesajili wakulima 5,156 ambao walikuwa hawajasajiliwa kwenye mfumo wa kupata mbegu ya ruzuku ambayo inatolewa na Serikali lakini kupitia maonyesho haya tumewasajili na sasa wataanza kunufaika na mbegu za ruzuku,” amesema Chimagu.

‎Amesema mfumo wa kusajili wakulima nchini ni mzuri kwani kwa kutumia mfumo huo wakulima wataanza kupata mbegu za mahindi za njia ya ruzuku ambalo ni asilimia 60 ya mazao ya nafaka yanayozalishwa nchini.

‎Amesema zao la mahindi kwa sasa linatambulika kama zao la biashara tofauti na hapo awali lilipokuwa linatambulika kama zao la chakula pekee na kwamba kuna masoko kadhaa nchini wamefunguliwa kwa ajili ya kuuza mahindi nje ya nchi.

“Kwa hiyo kama wakulima wataendelea kuuziwa mbegu feki ni wazi hatutaweza kufikia malengo yaliyowekwa ya kulisha bara la Afrika, msako bado unaendelea nchini wa kuwabaini wote wanouza mbegu bandia kwa wakulima ili tuwafikishe kwenye vyombo vya sheria,” amesema Chimagu.

‎Mkulima wa alizeti kutoka mkoani Singida, Elizabeth Shunda amesema mpango wa Serikali kutoa pembejeo za kilimo kama vile mbegu na mbolea zimechochea kwa kiwango kikubwa cha wakulima kulima kwa tija kwa sababu zinapatikana kwenye maeneo yao.

‎Shunda ametoa wito kwa wakulima nchini kujisajili kwenye mfumo wa wakulima ili wapate namba zao za usajili zitakazowawezesha kupata pembejeo hizo kwa mfumo wa ruzuku.

‎Hivi karibuni, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alizindua mfumo wa kuwasajili wakulima wa e-Kilimo ambapo mpaka sasa una wakulima takribani milioni 4 waliojisajili na lengo ni kusajili wakulima milioni 7 nchi nzima.

‎Bashe alisema lengo la kusajili wakulima ni kuwafahamu na kuwafikia popote walipo na kujua mahitaji yao ya mbolea, mbegu, huduma za ugani na huduma nyingine ambazo watazihitaji kwa wakati.