DROO ya michuano ya kimataifa kwa ngazi za klabu kwa msimu wa 2025-26 inafanyika leo mchana jijini Dar es Salaam, huku Yanga na Simba zinatarajiwa kukutana na miongoni mwa timu 16 katika hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa mujibu wa muongozo wa droo hiyo ambao Mwanaspoti limeunasa kutoka kwa mmoja wa maofisa wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Yanga na Simba kila moja inaweza kukutana na mojawapo kati ya Wiliete (Angola), Gaborone United (Botswana), US Zilimandjou (Comoro), AC Leopards (Congo), timu mbili za DR Congo, Nsingizini (Eswatini), Lioli (Lesotho) na Elgeco Plus ya Madagascar.
Nyingine ni Silver Strikers (Malawi), Cercle de Joachim (Mauritius), African Stars (Namibia), Remo Stars (Nigeria), Cot d’Or (Shelisheli), Power Dynamos (Zambia) na Simba Bhora ya Zimbabwe.
Kupangwa kwa Yanga na Simba kukutana na miongoni mwa timu hizo katika hatua ya awali kumetokana na kuwemo kundi la timu lililo katika nafasi za juu ya chati ya ubora wa klabu ya CAF kutokana na mafanikio zilizokusanya kwa kipindi cha misimu mitano iliyopita.
Miongoni mwa faida ambazo Yanga na Simba zitapata kwa kuwa katika nafasi za juu kwenye chati ya ubora ni kuanzia mechi za hatua hiyo ugenini na kumalizia nyumbani.
Katika chati hiyo ya ubora iliyotolewa na CAF jana, Simba ipo nafasi ya tano huku Yanga ikiwa katika nafasi ya 12.
Katika Kombe la Shirikisho Afrika, wawakilishi wa Tanzania, Azam FC na Singida Black Stars huenda wakakabiliana na timu mojawapo kati ya Etoile du Sahel ya Tunisia au klabu nyingine 17 kutoka mataifa mbalimbali.
Kwa vile Singida Black Stars na Azam hazina pointi zilizokusanya katika chati ya ubora wa klabu ya CAF, timu hizo zitaanzia hatua ya awali zikiwa nyumbani na zitamalizia ugenini.
Msimu uliopita Tanzania iliwakilishwa na Yanga na Azam katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga ilifika makundi wakati wenzao waliondoshwa mapema kama ilivyokuwa kwa Coastal Union iliyoshiriki Kombe la Shirikisho, wakiiacha Simba iliyocheza Shirikisho ikifika fainali na kupoteza kwa jumla ya ma bao 3-1 vs RS Berkane ya Morocco.