Ibenge aanza kuona mwanga Azam FC

KOCHA wa Azam FC, Florent Ibenge, ameonyesha imani na kuvutiwa na kiwango cha nyota wa timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ibenge alitoa kauli hiyo baada ya timu hiyo kushinda mabao 4-0 dhidi ya Arusha Combine katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa Black Rhino mjini Karatu, Arusha.

Azam kwa sasa, imeweka kambi ya maandalizi kwa ajili ya msimu wa 2025-2026, huku ikiwa na malengo makubwa ya kufanya vizuri katika Ligi Kuu, Kombe la FA na Kombe la Shirikisho Afrika.

“Nipo katika hatua ya kuwafahamu wachezaji wote, hivyo wanapaswa kuonyesha kuwa wana uwezo wa kucheza katika hii timu,” alisema.

Aliongeza, kila mchezaji anapaswa kuonyesha juhudi na uwezo alionao, ndio maana alitenga dakika 45 kwa kila mchezaji katika mchezo huo.

Kocha huyo raia wa DR Congo aliyejiunga Azam akitokea Al Hilal ya Sudan, alisema lengo ni kuandaa timu yenye ushindi kwa kuwafundisha wachezaji kutambua umuhimu wa kila mchezo wanaocheza.

Aliweka wazi ushindi dhidi ya Arusha Combine ni hatua moja tu kwenda katika kutimiza malengo waliyonayo, japo kocha huyo alikiri mchezo huo haukuwa na umuhimu mkubwa sana.

“Ni muhimu vijana wakimbie na lengo letu lilikuwa kuhakikisha wanakimbia angalau kilometa tano, wataendelea kufanya mazoezi ya kukimbia ili kuimarisha nguvu zao mwilini,”  alisema Ibenge.

Ibenge alisema, Azam inatarajia kucheza mchezo mwingine wa kirafiki ili kutathmini maendeleo ya wachezaji, ikiwemo maeneo ambayo yanahitajika kuboreshwa zaidi.