Mzenji mikononi mwa Pamba Jiji

MABOSI wa Pamba Jiji wanasuka kikosi hicho kimyakimya ili kuongeza ushindani msimu ujao, ambapo wako katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa beki wa kati wa Singida Black Stars, Mukrim Issa ‘Miranda’ kwa mkopo.

Nyota huyo kutoka Zanzibar msimu uliopita aliichezea Dodoma Jiji kwa mkopo pia akitokea Singida Black Stars, ambayo amebakisha nayo mkataba wa mwaka mmoja, japo mabosi wa kikosi hicho wanataka wamtoe kwa ajili ya kupata timu itakayompa zaidi nafasi.

Mwanaspoti linatambua, nyota huyo aliyeichezea Coastal Union kisha kujiunga na Dodoma Jiji anakaribia kutua Pamba, baada ya mabosi wa kikosi hicho cha ‘TP Lindanda’, kuvutiwa na uwezo wake na kuanza kufanya majadiliano ya maslahi binafsi.

“Mukrim bado ni mchezaji wetu halali wa Singida, ila tunataka kumtoa tena kwa mkopo, lengo ni kumpatia timu tunayoamini itampa nafasi zaidi ya kucheza katika kikosi cha kwanza na kuonekana kuliko tukimrejesha hapa,” kilisema chanzo hicho.

Tangu ajiunge na Dodoma katika dirisha dogo la usajili la Januari 2025, beki huyo ameonyesha uwezo mkubwa na kumpindua Mkongomani Heritier Lulihoshi aliyekuwa anacheza mara kwa mara, akitengeneza pia pacha nzuri na mwenzake, Abdi Banda.

Mbali na Pamba inayokaribia kuinasa saini ya nyota huyo, klabu mbalimbali zikiwemo Dodoma Jiji aliyoichezea msimu huu wa 2024-2025, Namungo na Mbeya City zote zilionyesha nia ya kumuhitaji.