BALOZI SIRRO AIPA MAUA YAKE EWURA KUWAFIKIA WAKULIMA, WAFUGAJI NANENANE

:::::::

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,  Balozi Simon Sirro ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Magahraibi kwa kuwafikia wakulima na wafugaji kwa kuwapa elimu na fursa mbalimvali za kuwaongezea kipato na thamani shughuli zao wakati wa maonesho ya Nanenane yaliyofanyika viwanja vya Ipuli Tabora kuanzia Agosti 1 hadi 8, 2025. 

 Sirro alitoa pongezi hizo Agosti 8 alipotembelea banda la EWURA wakati wa  kilele cha maonesho hayo kwa Kanda ya Magharibi iliyojumuisha mikoa ya Tabora na Kigoma na kueleza kuwa amefurahishishwa na ushiriki wa EWURA  ambao umekuwa chachu ya upatikanaji wa huduma za nishati na maji mchini.

“EWURA hongereni kwa kuwafikia wakulima na wafugaji, utaratibu huu uendelee na tuchape kazi”. Alisema. 

Meneja wa EWURA Kanda ya Magharibi, Walter Christipher, akitoa maelezo kwa kiongozi huyo, alisema kwamba zipo fursa za wakulima kuwekeza kwenye vituo vya mafuta maeneo ya vijijini ili kusogeza huduma akibainsha kuwa uhitaji wa huduma hiyo bado ni mkubwa, kadhalika fursa ya kujisajili kwenye kanzidata ya watoa huduma inayoratibiwa na EWURA ili kutoa huduma mbalimbali katika miradi mikubwa ya nishati na gesi asilia nchini. 

“ Katika maeonesho haya, tumewasisitiza wakulima na wafugaji kuzichukua fursa kama za kujenga vituo vya mafuta vijijini baada ya kuuza mazao na mifugo lakini pia kujisajili kwenye kanzidata, ili washiriki kutoa huduma katika miradi ya kimkakati nchini ya mafuta na gesi asilia mathalani mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Chongeani Tanga”. 

Aidha, alieleza pia kwamba, washiriki wa maonesho hayo wamesisitizwa kutumia nishati safi ya kupikia ili kutunza afya na mazingira ikiwemo kuwekeza katika biashara ya usambazaji wa LPG ambapo EWURA hutoa vibali na leseni kuwezesha shughuli hiyo.