Yanga yampandia ndege beki Msauzi

JANA, mabosi wawili wa ngazi za juu katika timu za Simba na Yanga waliziwakilisha katika droo ya mashindano ya Afrika, ambayo timu zao zinashiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Katika uchezeshwaji wa droo hiyo, rais wa Yanga, Hersi Said akiwa na mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ walihudhuria na kila mmoja alizungumzia chama lake linavyopanga kuweka rekodi katika mashindano hayo wakiapa ije mvua, liwake jua watatoboa katika hatua za awali dhidi ya wapinzani wao. 

Lakini, huku nyuma kama unadhani Yanga imefunga usajili, basi unakosema! Sikia, mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara bado wapo sokoni na sasa wanatafuta beki wa kati huku hesabu zao zikianzia kwa Mkongomani mmoja aliyewahi kutakiwa na watani zao, Simba.

Mabosi wa Yanga wameamua kumpandia ndege ili kufungua mazungumzo na beki Nathan Idumba Fasika anayeichezea Cape Town City ya Afrika Kusini, huku hesabu zao zikilenga kumnasa ili akakipige eneo la kati akishirikiana na mabeki waliopo kikosini ambao ni Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Dickson Job na Bakari Mwamnyeto.

Fasika ni beki wa viwango ambaye sio Yanga tu, bali hata Simba iliwahi kupambana kuinasa saini yake msimu uliopita, lakini ikakwama.

Yanga imetua kwa Fasika ikitaka aje kuongeza nguvu kwa kuwapa changamoto nahodha msaidizi, Job na Bacca.

Timu hiyo inapiga hesabu kwamba endapo ikitokea inamkosa mmoja kati ya Job na Bacca, isiwe na mashaka makubwa kwenye safu ya ulinzi kwani msimu uliopita ilitokea wakawa na ishu zilizowaweka nje kwa muda mfupi ambapo ilijikuta ikipoteza mchezo dhidi ya Tabora United kwa mabao 3-1.

Fasika ndani ya msimu uliopita nchini Afrika Kusini amekosa mechi mbili pekee za Ligi Kuu akicheza michezo 26 kati ya 28 ya msimu mzima.

Beki huyo Mkongomani amekuwa nguzo kubwa kwenye klabu yake ambayo ilimaliza katika nafasi ya 15 na kushuka daraja.

Licha ya timu yake kushuka daraja, lakini bado amekuwa akizivutia timu nyingi kutokana na ubora ambao amekuwa nao wakati wote anapokuwa uwanjani.

Yanga katika hesabu za kumpata Fasika itakuwa vitani kuwania saini yake sambamba na Golden Arrows ya Afrika Kusini inayomtaka atue kuichezea msimu ujao.

Taarifa za ndani ya Yanga zimelidokeza Mwanaspoti kuwa: “Fasika ni beki mzuri, unajua inayoshuka ni timu lakini haimaanishi kwamba kila mchezaji ni mbovu. Tunaendelea naye na mazungumzo.

“Tunataka kuwa na beki ambaye ataongeza changamoto pale kwenye eneo la ulinzi. Ukiangalia nahodha wetu (Bakari Mwamnyeto) ni kama amekubali kuwa chini ya Job na Bacca, sasa hii ni hatari kama akikosekana mmoja kati ya Job na Bacca.” Msimu uliopita, Mwamnyeto alikuwa mechi chache za mashindano.

Mwanaspoti liliwahi kuripoti kuwa Yanga iko katika harakati za kusaka beki wa kati ambaye atasaidiana na wazawa hao, lakini itaanza kwa kutazama michuano ya CHAN kuona kama itampata mtu anayestahili.

Mwishoni mwa msimu wa 2023/24, timu hiyo iliachana na beki wa kati Mganda Gift Fred baada ya kutoridhishwa na kiwango chake, hivyo kuifanya ibaki na walinzi watatu wa eneo hilo.