Mkongomani atajwa kumrithi Sowah Singida Black Stars

SINGIDA Black Stars (SBS) imeanza hesabu zake kwa mastaa wa kigeni na sasa inapambana kuziba nafasi ya Jonathan Sowah kwa kufuata mshambuliaji mmoja nchini DR Congo. Sowah ametimkia Simba katika dirisha hili la usajili linaloendelea.

Mshambuliaji ambaye Singida inamtaka ni Horso Muaku ambaye anaichezea FC Lupopo ya DR Congo.

Muaku ndiye mshambuliaji aliyepitishwa na kocha mpya wa timu hiyo, Miguel Gamondi, baada ya kumfuatilia Kenya katika michuano ya CHAN inayoendelea.

Mchezaji huyo anaitumikia nchi yake kwenye Fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), akiwa miongoni mwa wanaoanza katika kikosi cha kwanza.

Muaku alimchanganya Gamondi pale alipofunga bao la pili kwa DR Congo ilipoichapa Zambia kwa mabao 2-0, wiki hii.

Baada ya kupenyezewa taarifa hizo Mwanaspoti liliwasiliana na mmoja wa mabosi wa juu wa Singida anayeongoza mazungumzo hayo na tajiri wa FC Lupopo, Jacques Kyabula Kitwe, lakini hakupatikana na hata Gamondi.

Ingawa mazungumzo hayajafikia mwisho, lakini Mwanaspoti linafahamu hakuna ugumu kwa mabosi wa timu hizo kuuziana wachezaji kwani Singida Black Stars iliwahi kumnunua winga wa FC Lupopo, Manu Lobota.

Hata hivyo, bosi mmoja wa FC Lupopo aliliambia gazeti, “bado tunazungumza na Singida tukikamilisha nitakujulisha. Unajua Muaku bado ana mkataba wa miaka miwili hapa kwetu. Unajua hakuna ugumu marais wa timu zote hizi mbili ni watu wanaojuna, ni wanasiasa hawawezi kupishana sana na hii sio mara ya kwanza wao kuuziana wachezaji.”

Muaku amebakiza mkataba wa miaka miwili na Lupopo ambapo uliopita alifunga mabao 10 kwenye ligi nchini humo.