Katika jamii nyingi duniani, mjadala kuhusu nafasi ya mwanamume na mwanamke katika familia na kazi umekuwa ukizua maswali mbalimbali kuhusu usawa, wajibu, na haki.
Moja ya hoja ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara ni kama ni sahihi kwa waume kuwalipa wake zao mishahara kwa kazi wanazozifanya nyumbani au kwa mchango wao katika familia.
Fredrick Joshua, anasema hawezi kumlipa mkewe mshahara kwa kuwa yeye ni mwenza na si mfanyakazi wake.
” Kumlipa mshahara inaleta tafsiri mbaya kama vile ni kibaraka ama mtumishi wako na unamnunua.Kumlipa mshahara kutafanya mwanamke asiheshimiwe, na ndoa zisidumu, kwa sababu haitakuwa rahisi kuvumilia upungufu wake akikosea.
Kwa upande wake, Johari Shaaban ana mtazamo mwingine. Anasema kwa majukumu wanayofanya kinamama wanapaswa kulipwa.
“Wanatakiwa watulipe kwa sababu hata dunia ya sasa inasema mwanamke kazi yake kubwa ni kulea na kuzaa watoto. Pande zote za kidini na maisha ya dunia zinasapoti kwamba kazi yake kubwa ni kulea na kuzaa, hayo mambo sijui ya kupika, kuosha vyombo inatakiwa mwanaume na mwanamke wakubaliane awe anamlipa,” anasema na kuongeza:
“Lakini kwa sababu sasa hivi mambo ya dini tulishayaacha , ndio hivyo mtu anafanya tu, na kwa kwa dunia ya sasa ilipofikia ukija kusema mambo ya kulipwa italeta migogoro, lakini ni kweli inapaswa wanaume wawalipe wake zao kwa hizo kazi wanazozifanya.”
Hoja hii inaweza kuonekana ya kushangaza kwa baadhi ya watu, hasa katika jamii ambazo zimezoea kuona kazi za nyumbani na malezi ya watoto kama jukumu la kawaida la wanawake, bila malipo. Hata hivyo, suala hili linazua mjadala mpana kuhusu thamani ya kazi isiyolipwa, usawa wa kijinsia, na namna tunavyoona haki ndani ya ndoa.
Kwanza, ni muhimu kufahamu kuwa wanawake wengi wanaofanya kazi za nyumbani huchangia kwa kiasi kikubwa ustawi wa familia. Kazi hizi ni pamoja na kupika, kusafisha, kulea watoto, kusimamia bajeti ya nyumbani, na kuhakikisha kuwa maisha ya kila siku ya familia yanaendelea bila matatizo. Kazi hizi huchukua muda mwingi na mara nyingi hufanyika bila mapumziko au kutambuliwa kama mchango wa kiuchumi.
Katika hali hii, kuwalipa wake zao mishahara kunaweza kuwa njia mojawapo ya kutambua thamani ya kazi hii na kuleta usawa wa kiuchumi ndani ya ndoa.
Wapo wanaodai kuwa kulipa mishahara wake zao kunabadilisha maana ya ndoa kutoka kuwa uhusiano wa upendo na ushirikiano hadi kuwa mkataba wa kibiashara.
Hoja hii haina mashiko iwapo tutazingatia kuwa hata katika ndoa, uwiano wa haki na majukumu ni jambo muhimu. Ikiwa mume anafanya kazi nje ya nyumba na anapata kipato, huku mke akiwa anabaki nyumbani kufanya kazi zisizo na malipo lakini zenye thamani kubwa, basi kuwalipa wake zao ni njia ya kuhakikisha kuwa wote wanapata haki sawa kiuchumi. Hili halimaanishi kuwa ndoa inageuka kuwa biashara, bali ni kuthibitisha kuwa mchango wa kila mmoja unaheshimiwa na kuthaminiwa.
Aidha, katika baadhi ya familia, wake huacha kazi zao za kitaaluma ili kuweza kutunza familia. Uamuzi huu, ambao mara nyingi hufanywa kwa ajili ya ustawi wa watoto na familia kwa ujumla, huwa na athari kubwa kwa maisha ya kifedha ya mwanamke kwa muda mrefu.
Anapokatisha kazi yake, anakosa fursa ya maendeleo ya kitaaluma, mafao ya uzeeni, na uhuru wa kifedha. Kwa kuwalipa wake mishahara, waume wanaweza kusaidia kulipa fidia ya nafasi zilizopotea na kuhakikisha kuwa wake zao wanajenga maisha ya kifedha yasiyomtegemea mume pekee.
Kuna pia hoja za kisheria na kijamii zinazounga mkono wazo hili. Katika baadhi ya mataifa, sheria zimeanza kutambua kazi ya nyumbani kama mchango wa kiuchumi.
Katika kesi za talaka, mali ya ndoa hugawanywa kwa kuzingatia mchango wa kila mmoja, ikiwemo kazi zisizolipwa kama malezi na usimamizi wa nyumba. Hii inaonesha kuwa jamii na mifumo ya sheria inaanza kutambua kuwa kazi ya nyumbani ina thamani halisi. Ikiwa mfumo wa sheria unaweza kutambua mchango huu, kwa nini basi asiwe mume, ambaye ni mshirika wa karibu zaidi wa mke, naye akautambua na kuuthamini kwa njia ya malipo ya kifedha?
Wapo pia wanaopinga hoja hii kwa kusema kuwa mume na mke wanapaswa kushirikiana kwa hiari, na si kulipana mishahara, kwani wote ni familia moja. Hata hivyo, mtazamo huu unaweza kuficha hali halisi ya ukosefu wa usawa katika baadhi ya ndoa, ambapo mwanamke hufanya kazi nyingi zaidi za nyumbani bila msaada au utambuzi wowote.
Kwa kuweka utaratibu wa malipo au fidia, hii inaweza kusaidia kurekebisha mizani na kuhakikisha kuwa kila mmoja anathaminiwa. Aidha, hatua kama hizi huchochea majadiliano kuhusu mgawanyo wa kazi, haki, na wajibu katika familia, jambo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya jamii yenye usawa.
Kwa upande mwingine, suala hili linaweza kutekelezwa kwa njia mbalimbali ambazo hazihusishi mishahara ya moja kwa moja kama inavyotafsiriwa kwenye mazingira ya kazi ya kawaida.
Kwa mfano, mume anaweza kuhakikisha kuwa mke anapata sehemu ya mapato ya familia kwa ajili ya matumizi yake binafsi, uwekezaji, au hata kufungua biashara. Hii ni njia ya kumwezesha kiuchumi na kumwezesha kujitegemea kifedha, bila kuhitaji kumlipa mishahara kama mfanyakazi.
Kwa wengine, kuwapa wake zao usaidizi wa kifedha kwa kazi wanazofanya siyo suala la mishahara tu, bali ni ishara ya kuthamini na kuonyesha shukrani.
Pia, tunapaswa kuzingatia athari ya kiakili na kihisia kwa wanawake wanaofanya kazi ya nyumbani kwa muda mrefu bila kutambuliwa.
Tafiti nyingi zimeonyesha kuwa wanawake wanaofanya kazi hizi bila msaada au utambuzi mara nyingi hukumbwa na msongo wa mawazo, uchovu wa kudumu, na hata hisia za kutothaminiwa.
Kwa hivyo, kuwalipa wake mishahara au kuwawezesha kifedha ni mojawapo ya njia za kuboresha afya ya akili na ustawi wa wanawake ndani ya ndoa.
Hata hivyo, si familia zote zina uwezo wa kifedha wa kutoa mishahara ya wazi. Katika hali kama hizi, mazungumzo na makubaliano ya wazi kuhusu mgawanyo wa kazi, usawa wa rasilimali, na kusaidiana kwa heshima ni muhimu zaidi.
Malipo haya yaweza kuwa kwa njia ya kupeana muda wa kupumzika, kusaidiana katika majukumu, au kupanga pamoja malengo ya kifamilia kwa kuzingatia mchango wa kila mmoja.
Kwa kumalizia, suala la mume kumlipa mke wake mshahara si la kifedha tu bali ni la maadili, usawa, na kutambua mchango wa kila mmoja katika familia. Ni njia mojawapo ya kuleta heshima, usawa na mshikamano ndani ya ndoa.
Ingawa si lazima iwe mishahara kwa maana ya malipo ya kila mwezi kama kazini, kuweka mfumo wa kutambua na kuthamini kazi ya mke ni hatua muhimu kuelekea familia yenye haki na usawa.
Ni wajibu wa kila jamii kufikiria upya thamani ya kazi zisizolipwa na kuhakikisha kuwa hakuna anayebeba mzigo wa kazi kwa jina la mapenzi bila msaada wala utambuzi.
Ingawa jambo hili linaweza kuonekana kama njia ya kuthamini mchango wa wanawake katika familia, kwa mtazamo wa kina, si sahihi kudai au kutekeleza mfumo wa mume kumlipa mke wake mishahara. Hii ni kwa sababu ndoa si taasisi ya kibiashara, bali ni muunganiko wa watu wawili kwa msingi wa upendo, ushirikiano, na kujitolea kwa hiari.
Kwanza, msingi mkuu wa ndoa ni ushirikiano, si biashara. Ndoa ni taasisi ya kijamii ambapo watu wawili huamua kuungana na kushirikiana maisha yao kwa mapenzi na heshima. Kwa hiyo, kuingiza wazo la mishahara katika mahusiano ya ndoa kunapotosha maana halisi ya ndoa.
Sheikh wa Mkoa wa Tabora, Alhaj Ibrahimu Mavumbi, anasema Uislam kwa anavyojua yeye hauna mafundisho rasmi yanayomlazimisha mume kumlipa mshahara mkewe.
“Sijawahi kukutana na hadithi (maelezo ya Mtume Muhammad- Rehma na amani vimshukie) inayosema hivyo mume amlipe mke mshahara. Elimu ya dini ni pana, inawezekana ikawepo lakini mimi ninachojua zipo kazi ambazo mwanamke akizifanya kumfanyia mume wake, inahesabika kwamba ni hisani ya mwanamke kwa mwanaume. Sasa kama mwanaume ataamua kumfanyia hisani mke wake kwa kulipa yale anayoyafanya hilo siyo baya,” anasema na kuongeza:
Mfano katika dini ya Kiislamu kuna kitu kinaitwa rai. Rai ni jambo zuri ambalo mtu anaweza akalifanya la halali ambalo halileti madhambi katika Uislamu wala Mtume (Rehma amani zimshukie) hajakataza. Ndio mfano mimi mke wangu nimeona ananifanyia kazi, ananipikia, ananifulia nguo, ananinyooshea pasi, anasafisha nyumba, nimeamua mimi kuwa nampa kila mwezi Sh40,000 ama 50,000 wala siyo haramu wala haijakatazwa kwavile anachokifanya hicho sicho kilichomleta katika ndoa yake.”
Anasema Mtume (Rehma na amani zimshukie) katika maisha yake, alikuwa anafanya kazi za ndani ya nyumba kama kufagia, kuosha vyombo, kufua tofauti na sasa watu wamegeuza wanawake kuwa kama ndiyo wafanyakazi wao.
Naye Katibu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Mkoa wa Mwanza, Mchungaji Emmanuel Sangosango, anasema si vibaya kwa mwenza kumwezesha mwenzake kiichumi.
“Jinsi ilivyo kwenye sheria ya ndoa kiserikali na kidini, tunasema kwamba moja ya majukumu ya wanandoa ni kutunzana. Kwa kuwa wanaume wapo kwenye njia za kiuchumi tunashauri wawawezeshe wake zao kiuchumi, na inapokuwa upande wa mwanaume anakosa uwezo wa kuitunza familia kwa ugonjwa wa muda mrefu au ajali amekuwa ni wa kitandani, jukumu linahamia upande wa mke wake kuitunza familia na kumtunza huyu baba,”anasema na kusisitiza wanaume kuwawezesha kiuchumi wake zao, ikiwamo kuwaruhusu kuajiriwa.