Ndugai alikuwa zawadi kwa wazazi, Taifa

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kondoa, Given Gaula amemtaja Spika wa Bunge mstaafu, Job Ndugai kuwa zawadi kwa wazazi wake, mkewe, wanawe na Taifa la Tanzania.

Enzi za uhai wake, amesema Mungu amemtumia Ndugai kwa namna ya ajabu na ameacha alama hata kwa wanaomkosoa wataangalia zaidi upande wa haki ili kufafanua maisha yake.

Askofu Gaula ameyasema hayo leo, Jumapili Agosti 10, 2025 alipohubiri kwenye hafla ya kitaifa ya kuaga mwili wa Ndugai inayofanyika katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma na kuhudhuriwa na waombolezaji mbalimbali akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika maelezo yake wakati wa ibada, Askofu Gaula amesema Ndugai aliyefariki dunia Agosti 6, 2025 jijini Dodoma pia alikuwa zawadi kwa Kanisa la Anglikana, alilolinyenyekea muda wote.

“Katika Dayosisi ya Kondoa ambako mimi natoka, Job alikuwa mnyenyekevu kweli, hata ningemwalika hakuwahi kutoa udhuru, hata angekuja kwa kusali tu,” amesema.

Amesema kuna siku Ndugai alipiga magoti muda mrefu kiasi cha mmoja wa watenda kazi kuhoji kwa nini imekuwa hivyo, lakini yote ni ithibati kuwa alikuwa mnyenyekevu.

Ameeleza mema yaliyofanywa na Ndugai enzi za uhai wake, yataendelea kuishi na kukumbukwa katika mioyo ya binadamu wengine.

“Wengine tukipata vyeo hata ibada hatukumbuki, lakini Job alikuwa mtu wa ibada. Wengine Mungu akikuinua basi,” amesema.

Baada ya shughuli hiyo kumalizika, mwili wa Ndugai utapelekwa viwanja vya Kongwa ili kutoa fursa kwa wananchi kumuaga mbunge wao wa zamani aliyewaongoza kwa zaidi ya miaka 20.

Mwili wa Ndugai unatarajiwa kuzikwa kesho Jumatatu, Kongwa. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ndiye anatarajiwa kuongoza mazishi hayo.

Endelea kufuatilia Mwananchi