Dk Tulia: Wanaoisifu kazi ya Ndugai ni wengi kuliko wanaobeza

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson amesema maisha ya kujitolea ya Spika mstaafu, hayati, Job Ndugai (62) yanasifiwa na wengi, kuliko idadi ya wanaoyabeza.

Ametumia maneno hayo pia, kumweleza Rais Samia Suluhu Hassan kuwa, walio upande wake ni wengi kuliko waliopo kinyume naye, hivyo hapaswi kuogopa.

Dk Tulia ameyasema hayo leo, Jumapili Agosti 10, 2025 alipotoa salamu za Bunge katika hafla ya kitaifa ya kuaga mwili wa Ndugai aliyefariki dunia Agosti 6, 2025 baada ya kuugua ghafla shinikizo la damu, lililosababishwa na maambukizi makali kwenye mfumo wa hewa.

Amemzungumzia Ndugai kuwa, kazi nzuri ya kujitolea aliyoifanya wengi wanaisifu kuliko wanaobeza.

Ametumia maneno hayo pia kumweleza Rais Samia kuwa, jana Jumamosi ameshuhudia watu wengi waliomuunga mkono katika uchukuaji fomu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ya kuwania urais, ni ishara kwamba walio wengi wapo upande wake.

“Nikutie moyo mheshimiwa Rais, ninayo imani kwamba jana umeona wana Dodoma walivyojitokeza kwa wingi kukuunga mkono, hiyo ni kuonyesha kwamba walio upande wako ni wengi kuliko walio kinyume nawe. Na sisi tulio upande wako ni wengi kuliko walio kinyume nawe, hivyo usiogope.

Sambamba na hayo, amesema Ndugai alikuwa si kiongozi wa kisiasa, bali mwalimu wa nidhamu, mlezi wa mshikamano na mtetezi thabiti wa haki.

Amesema alielewa kwa undani kwamba uongozi si heshima ya vyeo bali ni wito na wajibu wa kujitoa kwa dhati kwa ajili ya wengine na aliyaishi maandiko ya Mungu.

“Alisimama kidete kuhakikisha kwamba kila sauti ndani ya Bunge, bila kujali chama au eneo alilotoka mtu inasikilizwa na kuthaminiwa. Wengi wetu na hapa nasisitiza neno wengi, tumeshuhudia mema ya marehemu alituongoza, tulimsikiliza, tunajifunza kutoka kwake,” amesema.

Amesema alikuwa mbunifu na alisababisha mageuzi mengi ya utendaji ndani ya Bunge.

Katika kipindi chake, amesema ndipo ugonjwa wa Uviko-19 aliposhamiri na akaanzisha vikao kwa njia ya mtandao, vinavyoendelea hadi sasa.

Amesema alikuwa mwalimu wake na msisitizo wake ulikuwa ni kuwa na Bunge linaloishauri na kuisimamia Serikali kwa uwazi, kwa masilahi ya wananchi sio kelele bali hoja na maadili.

“Kauli hizi zilikuwa dira katika kufikia malengo tuliyojiwekea na kuhakikisha Serikali inaendelea kuwezesha ustawi wa wananchi wote,” amesema.

Mwili wa Ndugai utazikwa kesho Jumatatu Agosti 11, 2025 Kongwa, mkoani Dodoma.

Endelea kufuatilia Mwananchi