Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametaka kujengwa makumbusho yatakayoeleza mchango wa Wilaya ya Kongwa katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, ikiwa ni sehemu ya kuenzi ndoto za Spika mstaafu, hayati Job Ndugai.
Agizo hilo la Rais Samia, linatokana na kile alichoeleza, kiongozi huyo wa zamani wa muhimili wa Bunge, alitamani mchango wa Kongwa uendelee kutambulika katika historia hiyo, hivyo ni vema hilo litekelezwe.
Ndugai amefariki dunia saa 9 alasiri ya Agosti 6, 2025 alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua kwa muda mfupi, maradhi ya shinikizo la chini la damu, lililosababishwa na maambukizi makali kwenye mfumo wa hewa.
Rais Samia ameyasema hayo leo, Jumapili Agosti 10, 2025 alipohutubia waombolezaji katika hafla ya kuaga mwili wa Ndugai iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

Amesema enzi za uhai wake, Ndugai alitamani kuutangaza mchango wa Kongwa katika harakati za kupambania uhuru wa Kusini mwa Afrika na alitaka kujengwe makumbusho ya Taifa na programu ya urithi huo.
“Maono ambayo ni vema yakafanyiwe kazi ili mchango wa Kongwa kwenye ukombozi wa Kusini mwa Afrika utambulike vizuri zaidi. Kwa wale wenye sekta zinazohusika katika kumuenzi ndugu yetu huyu, hilo naomba lifanyiwe kazi,” amesema.
Katika hotuba hiyo, Rais Samia amemtaja Ndugai, alikuwa kiongozi mkomavu kisiasa na kiuongozi na aliamini katika demokrasia ya Bunge, ndiyo maana aliaminiwa katika nyadhifa mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Amesema jitihada zake, ziliwezesha kukamilisha jengo la utawala la Bunge, lililoongezeka kumbi za mikutano ndani yake na hivyo kuepusha gharama za vikao vya kamati kukodi kumbi za nje.
Rais Samia amesema Ndugai atakumbukwa kwa kuwa mwanasiasa aliyependa maendeleo ya vijana hasa kuhakikisha wanapata elimu.
“Ametuachia faraja kwamba miongoni mwa aliopenda wapate elimu ya uhakika walikuwa ni wasichana, ndiyo maana alijitolea mwenyewe kusimamia upatikanaji wa fedha za kujenga shule ya wasichana Bunge iliyopo Kikombo Dodoma,” amesema.
Amesema Ndugai atakumbukwa sio tu kwa kuiwezesha Kongwa kutoa kiongozi mkuu wa muhimili, bali kupambania maendeleo ya watu wake, ndiyo maana alipokwenda kuomba ridhaa alipewa na wananchi.

Ameeleza mwaka 2000 Ndugai alipoanza kuwa Mbunge wa Kongwa ilikuwa na Shule za Msingi 50, lakini sasa zimefikia 131, sekondari tatu, sasa 45, vituo vya afya vitatu, sasa 10 na zahanati 12 na sasa 56, huku umeme ulikuwa katika vijijini 10 lakini sasa kote.
“Maendeleo haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na msukumo wake na namna alivyopambania Kongwa. Nakumbuka nikiwa Makamu wa Rais nilikuwa nafanya ziara Dodoma nikasimama Kongwa, akasema umeme hauna uhakika Kongwa, akaomba kituo cha kupooza umeme tukamjengea na sasa umeme unapatikana,” amesema.
Rais Samia amesema Ndugai akiwa hai alipata heshima ya kuwekewa alama ya jina lake litakalobaki milele katika Soko la Job Ndugai.