Kamanda Muliro ang’aka wezi wa pikipiki Dar, atangaza kiama

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imetangaza kuwavalia njuga wizi wa pikipiki baada ya kuwakamata watuhumiwa wanne wakiwamo wanaohamasisha wizi wa vyombo vya moto na kuuza kwa bei ndogo.

Watuhumiwa wengine kati ya hao, wamekamatwa baada ya kudaiwa kuvamia na kuvunja nyumba ya mfanyabiashara raia wa China na kupora Sh105 milioni.

Kati ya fedha hizo zilizoporoshwa, Polisi imesema Sh82 milioni zimekamatwa kutoka kwa watuhumiwa hao na zingine tayari watuhumiwa walishaanza kutumia kununua viwanja na kuweka kwenye simu na kufyatua matofali.

Hayo yamesemwa leo Jumapili, Agosti 10, 2025 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alipozungumza na waandishi wa habari.

Amewataja waliokamatwa kwa tuhuma za kuhamasisha wizi wa pikipiki maeneo ya Tabata Agosti 8, 2025 ni Hamad Mohamed (49), mkazi wa Kigogo na Abdul Ramadhani (20) mkazi wa Yombo.

“Hatua ya awali, tumewakuta na pikipiki mbili wakiwa kwenye harakati za kuziuza, upelelezi zaidi unaendelea, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lina hakika watu wote ambao wamekuwa wakihusika na wizi wa pikipiki tutawakamata.

“Kumekuwa na kikundi cha watu wanaonunua kwa bei rahisi na wao kuziuza kwa bei rahisi, biashara hiyo itawapa matata, hawa waliokamatwa watakuwa mfano katika kuwashughulikia kwa kutumia mifumo ya sheria kuhakikisha biashara hiyo hailipi,” amesema Kamanda Muliro.

Kamanda huyo amesema jeshi halitakubali watu kufanya biashara isiyo halali, hivyo kama ambavyo biashara ya wizi wa vifaa vya magari ulivyokomeshwa ya pikipiki nayo itakomeshwa.

“Wananchi wasisitize kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na wizi hasa pikipiki na kuacha madhara kwa watu wengine taarifa hizo tutazifanyia kazi na biashara hii tutaikomesha,” amesema.

Katika hatua nyingine, Kamanda Muliro amewataja Mathias Charles (24), mkazi wa Salasala Kinondoni Dar es Salam na Kassim Abdallah (30), mkazi wa Tegeta kushikiliwa na kwa tuhuma za wizi wa fedha mali za mfanyabiashara raia wa China.

Kamanda Muliro amesema watuhumiwa hao walivunja nyumba ya mfanyabiashara huyo na kuingia ndani kupitia chooni na kupora kiwango hicho cha fedha na kutokomea nazo.

“Baada ya tukio hili walitoweka kwenda maeneo tofauti tofauti na Jeshi la Polisi liliendelea na ufuatiliaji na hatimaye walikamatwa wakahojiwa kwa kina na baadaye walikiri maeneo walikoweka fedha hizo.

“Sh82 milioni na Dola 267 zimepatikana, lakini zingine tayari walishazifanyia manunuzi mbalimbali ikiwamo viwanja na kufyatua matofali,”amesema.

Kamanda Muliro ameonya watu wote wanaojihusisha na matukio ya uhalifu kuachana nao mara moja kwani matukio hayo hayalipi.