KIPA wa zamani wa kimataifa aliyewahi kuwika na timu za Simba, Yanga, Azam pamoja na Taifa Stars, Deogratius Munishi ‘Dida’ kwa sasa akijulikana kama Yunus baada ya kusilimu, amezungumzia suala hilo huku akimtaja mchezaji mwenzake Elias Maguri kuwa ni watu waliochangia kufanya uamuzi.
Kipa huyo alisema imemchukua muda mrefu kufanya uamuzi huo, baada ya Maguri aliyewahi kutamba na timu kadhaa zikiwamo Simba, Stand United na Taifa Stars, alikuwa akimpa mawaidha na kumfunulia hadithi na mafundisho ya dini hiyo kabla ya kubadili dini, huku akiwataka Watanzania kutambua amebadili dini bila kishawishi chochote bali kwa imani.
“Kuna wengine wanakuwa na mawazo potofu kwamba labda nimepata mke mwingine ndio maana nimeamua kufanya hivyo, bado nipo na mke wangu yule yule na watoto wangu wawili na hakuna tukio lililosababisha hilo,” alisema Yunus na kuongeza;
“Nilifanya uamuzi huo binafsi, maana ni imani ya mtu binafsi, baada ya kurejea nyumbani mke wangu alishituka lakini baadaye akakaa sawa, nikitulia nitamwelezea ili ajiunge na mimi mume wake, ila kuhusu watoto watafanya uamuzi wao bila kuwalazimisha maana mimi sijalazimishwa.
“Nilijiunga na Geita Gold dirisha dogo msimu uliopita, nikakutana na Maguri niliyekuwa nakaa naye chumba kimoja, alikuwa ananisimulia hadithi nzuri za mtume na alikuwa ananiambia nikiingia dini hiyo nitajisikia vizuri, ila nilikuwa najibu ‘Inshaallah’ na sasa imekuwa, mbali na Maguri kuna wachezaji wengi walikuwa wananishauri niingie dini hiyo.”
Alisema ieleweke alipokuwa Mkristo hakuwahi kufanya matukio ya aina yoyote ya kashfa, hivyo muamuzi wake hauhusiani na kuona dini nyingine haina haki.
“Katika kanisa nililokuwa nasali ni mkristo mmoja ambaye kanitumia ujumbe katika simu yangu wa hongera Mungu ni mmoja na anitangulie na sasa natenga muda wa kumueleza mama kuhusiana na hilo,” alisema kipa huyo aliyewahi pia kuzitumikia Mtibwa Sugar, Mbeya City na sasa yupo Geita.
Dida sio mchezaji wa kwanza nchini kubadili dini kwani hata Clement Mzize naye mwaka jana alitangaza kubadili dini akiitwa jina jipya la Walid mbali na wale wa kimataifa ambao wamekuwa wakitangazwa hadharani.