Pemba. Watiania wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar wamemaliza kujitambulisha kwa wananchi wa Zanzibar huku wakisema wako ‘fiti’ kuanza mchakato wa kampeni za siku 60 za kuhakikisha wanaibuka kidedea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kampeni za uchaguzi mkuu zitaanza Agosti 28 hadi Oktoba 28 kisha siku inayofuata kupiga kura.
Katika maelezo yao, wamesema muunganiko wa Luhaga Mpina (mtania urais Tanzania) na Othman Masoud (Zanzibar) wanakwenda kutimiza maono ya Watanzania na kuisuka Zanzibar yenye mamlaka kama alivyokuwa akiitaka marehemu Maalim Seif Sharif Hamad (mwenyekiti wa zamani wa chama hicho).
Wameeleza hayo leo Jumapili, Agosti 10, 2025, wakati wakihitimisha mchakato wa kujitambulisha kwa wananchi wa Pemba baada ya kupitishwa na mkutano mkuu wa chama hicho, Agosti 6, 2025, jijini Dar es Salaam, kuwania tiketi hiyo.

Utambulisho wa watiania hao ulianzia jana Jumamosi mjini Unguja, Agosti 9, 2025, ambapo walipokelewa na umati wa wananchi. Kama ilivyokuwa Unguja, Pemba nako umati wa watu waliojitokeza pembezoni mwa barabara kuanzia uwanja wa ndege hadi Tibirinzi, wakiwa na mabango yenye jumbe mbalimbali.
Hata hivyo, CCM kupitia kwa mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, jana Jumamosi akichukua fomu ya kuwania urais, alisema wamejipanga kuendelea kushinda uchaguzi na kila kitu kimekamilika.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, alisema silaha mbili watakazozitumia ni Ilani ya 2020/25 jinsi ilivyotekelezwa kwa mafanikio makubwa na ilani ya 2025/30 inavyoeleza watakavyokwenda kuifanya Tanzania maendeleo makubwa.

Akiwahutubia mamia ya wananchi katika mkutano visiwani Pemba, Mpina amedai Taifa bado linakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo upatikanaji wa Katiba mpya, suala la Muungano, lakini ACT Wazalendo ina watiania hodari watakaowatoa Watanzania kwenye mkwamo huo.
“ACT Wazalendo imewaletea vijana hodari, wapo kamili na tayari, kutatua kero za Muungano na tupo fiti kuziomba kura muda ukifika kuanzia kwenye kijiji, vitongoji, matawi, kata, majimbo hadi mikoa.
“Siku 60 za kampeni ni chache sana kwetu, tunaweza kufanya kampeni siku zaidi ya 180, maana yake tukiwango’a CCM ndani ya siku hizo tutakuwa hatujachoka,” ameeleza Mpina, mbunge wa zamani wa Kisesa huku akishangiliwa.
Mpina, aliyewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, amesema ACT Wazalendo Oktoba inakwenda kuing’oa CCM madarakani, akisema hivi sasa ushindi wa Zanzibar hautaishia njiani tena.
“Muda ukifika tutakwenda kila kona ya nchi kueleza umma, tumezaliwa kwa ajili ya Watanzania, hatukubali kuona wananchi wakinyanyasika wakati tupo sisi vijana,” amesema Mpina.

Naye mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman, amejinasibu kuwa anayejua changamoto za Wazanzibari, hivyo amewaomba wananchi wa visiwa hivyo kuwaunga mkono katika uchaguzi Oktoba na chama hicho kipo tayari.
“Nimelelewa katika maisha ya kuwatumikia wananchi, kupitia malezi ya watu mbalimbali waliokuwa serikalini, ndio maana najua changamoto za watu,” amesema Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar.
“Nimekuzwa na kulelewa na wanaojua Zanzibar, sasa nipo tayari kuwatumikia wananchi wa Pemba na Unguja. Sasa hivi tunajiandaa kuingia chumba cha upasuaji (kujiandaa na uchaguzi),” amesema Othman ambaye hotuba yake ilijikita kwenye mafumbo ya kupiga vijembe CCM.
Kwa upande wake, mgombea mwenza wa urais wa Tanzania, Fatma Abdulhabib Ferej, aliyewahi kushika wadhifa wa uwaziri Zanzibar, amesema Mpina ni mmoja wanasiasa msema kweli na katika misimamo yake huwa hapindishi maneno.
Amewataka wananchi wa Zanzibar kuhalikisha wanaitoa CCM kuanzia katika majimbo ili chama hicho tawala kikose wawakilishi na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Naye kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema viongozi wa chama hicho walifanya tathmini ya kina hadi kumpa kijiti Mpina cha kuwania urais, akiwataka wanachama wao kutokuwa na wasiwasi na mtiania huyo.
Kutokana na hofu na shaka walizonazo, Zitto amewaambia Wazanzibari kuwa viongozi wa chama hicho wanabeba dhamana kuhusu ujio wa Mpina ambaye amepitishwa kuwania urais wa Tanzania.
Katika maelezo yake, Zitto amesema anaelewa wasiwasi wa wananchi wa Zanzibar, uliotokana na historia ya hapo nyuma ya watu waliohamia chama hicho, lakini mambo yalikuwa tofauti na matarajio ya chama hicho.
Zitto amesema anamjua vyema Mpina tangu walivyokutana naye kwa mara ya kwanza mwaka 2005 bungeni na kufanya kazi kwa pamoja za kibunge hadi mwaka 2020.
“Mpina akikwambia nyeupe ni nyeupe, akikwambia nyeusi ni nyeusi. Naelewa na viongozi wenu wanaelewa, wasiwasi wenu wa huko tulikotoka. Lakini tumefanya tathmini ya kutosha, tunamchukulia dhamana Mpina kwa sababu tunamwamini.
“Historia yake ni mwanasiasa mwenye msimamo, anayechukizwa na ufisadi na ubadhirifu katika Taifa letu. Ni historia ya mwanasiasa anayetaka kuona mabadiliko katika Taifa, aliyeamua kuungana na wenzake ili kutekeleza wajibu muhimu sana,” amesema Zitto.