Wagombea urais NLD, Makini, UPDP waanika vipaumbele vyao

Dodoma. Wagombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameendelea kuchukua fomu huku wakianika vipaumbele na mikakati ya kuwapeleka Ikulu.

Leo Jumapili, Agosti 10, 2025, ilikuwa siku ya pili tangu pazia la kuchukua fomu hizo lilipofunguliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), na mpaka sasa jumla ya vyama sita vimeshachukua fomu.

Wagombea waliochukua fomu na vyama vyao kwenye mabano ni Samia Suluhu Hassan (CCM), Kunje Ngombale (AAFP), Hassan Almas (NRA). Leo waliochukua fomu ni Coaster Kibonde (Chama Makini), Doyo Hassan Doyo (NLD), na Abdallah Kadege wa UPDP.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na INEC, uchukuaji fomu ulioanza Agosti 9, 2025, utahitimishwa Agosti 15, 2025 kwa awamu ya kwanza, kabla ya wagombea wote wa vyama 18 vilivyothibitisha kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuanza safari ya kusaka wadhamini mikoani.

Aliyefungua mlango wa INEC kwa siku ya leo na kupokelewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhana Kailima, alikuwa ni Doyo Hassan Doyo, aliyefuatiwa na Coaster Kibonde na Twalibu Kadege, huku kila mmoja baada ya kukabidhiwa fomu akiahidi kushinda na kuunda serikali imara itakayokuwa mkombozi kwa Watanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari, mgombea wa NLD, Doyo, amesema siku ya kwanza akishaapishwa atapiga mnada mashangingi yote ya Serikali na kununua magari yasiyozidi Sh30 milioni kwa kila moja akisema lengo ni kubana matumizi.

Mgombea huyo amesema magari ambayo watayatumia watumishi wa Serikali gharama yake haitazidi Sh30 milioni.

“Hata mimi mwenyewe nitatembelea gari la thamani hiyo hiyo,” amesema.

Doyo, ambaye amefika ofisi za INEC akiwa amepanda bajaji, ameeleza namna chama hicho kilivyojipanga kuondoa matumizi yasiyo ya lazima katika Serikali ili Watanzania wanyonge wapate ahueni ya maisha.

Msafara wa mgombea huyo ulikuwa na magari manne yenye wapambe, akiwamo mgombea mwenza wake, Chausiku Khatibu Mohamed, na pikipiki chache zilizokuwa zikipiga hodi na kuwasha taa.

“Mfano hili la ajira, siendi kupunguza bali nakwenda kumaliza kabisa tatizo la ukosefu wa ajira. Haiwezekani tukawa na vijana waliomaliza vyuo vikuu zaidi ya miaka mitatu, halafu hawana ajira,” amesema Doyo.

Kwa upande mwingine, mgombea huyo amesisitiza suala la kilimo akiwaahidi vijana kuwa kila mtu atamiliki ekari tano na zitalimwa kwa kutumia mitambo ya kisasa yakiwamo matrekta. Amesema kilimo cha jembe la mkono kinaumiza wengi.

Akizungumzia tozo, amesema NLD kinakwenda kuzifuta kwa wajawazito sambamba na gharama maiti wanazodaiwa ndugu mara wagonjwa wao wakifariki dunia wakiwa wodini wamelazwa huku wanadaiwa fedha za matibabu.

“Hili la kudai fedha ndipo mruhusu maiti, ni aibu kubwa. Nasema hivyo kwa sababu kaka yangu alipoteza maisha tukakuta tunadaiwa karibu Sh7 milioni ndipo tupewe mwili. Tulichanga hadi Sh2 milioni lakini wakagoma, lazima nikomeshe hayo mambo,” amesema bila kufafanua kama maiti huyo walikabidhiwa au hapana.

Amesema Serikali atakayoiongoza itakuwa na vipaumbele vinne ambavyo ni elimu, afya, ajira, na miundombinu, akisisitiza watajenga barabara ya njia nane Dar es Salaam hadi Chalinze ambako watajenga bandari kubwa kwa ajili ya kuenzi uongozi wa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Mgombea urais wa Chama cha Makini, Kibonde, baada ya kuchukua fomu, ameainisha mambo matatu aliyotaja kuwa ndiyo kilio kikuu cha Watanzania.

Kibonde, ambaye alifika INEC akiwa na msafara wa magari matatu na wapambe wachache waliovalia sare za chama chao, alikaribishwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima na kumuelekeza ukumbini zilikokuwa zinatolewa fomu hizo.

Baada ya kukabidhiwa fomu, Kibonde amesema chama hichi tayari kina vipaumbele vitatu vya elimu, kilimo, na afya vitakavyowaongoza katika kujinadi kwenye kampeni zao.

“Naamini Oktoba tunakwenda kushinda kiti cha Rais na kutinga Ikulu. Tumekusudia kuunda Serikali ambayo itakuwa ya matumaini, kila Mtanzania ataifurahia.

“Tunataka kumaliza kero zinazowakabili Watanzania, hivyo naahidi tutakwenda kuunda serikali makini,” amesema Kibonde.

Akizungumzia kipaumbele cha elimu, amesema kumnyima elimu mtoto wa Kitanzania ni sawa na kumpa kifungo cha maisha, lakini mtu akinyimwa afya ni sawa na kumhukumu hukumu ya kifo.

“Kwa hiyo kwenye afya tunakuja na kitu kinaitwa Care Makini, ambayo ni bima ya afya kwa wote, na tutajenga vituo vya afya vya kisasa kila kata, lakini kilimo tutahakikisha kila kijana anapatiwa ekari tano ili alime kisasa,” amesema Kibonde.

Hata hivyo, amesema katika safari ya kuisaka Ikulu, wamejenga matumaini makubwa kutoka kwa INEC kwa namna ilivyowashirikisha, wakiamini kuwa watangazwa baada ya kushinda uchaguzi wa Oktoba 2025.

Kwa upande wao, Chama cha UPDP kimesema bado hakijazindua ilani yake, lakini wanaamini katika mambo matatu.

Mgombea wa chama hicho, Twalibu Kadege, ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kukabidhiwa fomu na INEC na kueleza kwa sasa anaanza hatua ya kusaka wadhamini kabla ya mambo mengine.

Kadege amesema muda wowote watazindua ilani yao ya uchaguzi ambayo imebeba mambo mengi yenye furaha ndani yake, huku akijinasibu kuwa anaamini Watanzania watawachagua kwa namna nzuri na kushinda katika uchaguzi mkuu.

“Lakini kwa sasa tuna mambo matatu, nayo ni ardhi, afya, na uhuru wa vyombo vya habari hasa maeneo ya vijijini. Kikubwa wananchi watupe ridhaa ili wakafurahie hiki tulichodhamiria kukitenda,” amesema Twalibu.

Kwa mujibu wa Kadege, kila kitu kinategemea ardhi, hivyo wakiwekeza nguvu kubwa katika eneo hilo, wanaamini watagusa makundi mengi likiwamo la Watanzania wanyonge.

Mgombea huyo na mgombea mwenza wake, Abdallah Mohamed Hassan, wameingia katika ofisi za INEC wakiwa kwenye bajaji wazi na wapambe wachache.

Miongoni mwa vyama vilivyoingia na wapambe wachache ni cha UPDP, na mgombea wake ndiye aliyezungumza kwa kutumia muda mfupi zaidi.

Alipomaliza kuzungumza na waandishi wa habari, Kadege aliwaita wapambe wachache alioongozana nao wakapanda magari matatu ambayo yaliingia yakiwa nyuma ya bajaji, huku bajaji waliyoingia nayo ikiondoka na dereva pekee.