JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limekamata shilingi milioni 82 za wizi na dola za Marekani 267, ambazo ziliibwa nyumbani kwa Xue Huaxion, Mkurugenzi wa Kampuni ya Huaren iliyopo Salasala, Wilaya ya Kinondoni.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Jumanne Muliro, alisema kuwa Julai 27, mwaka huu, walikamatwa watuhumiwa wawili — Mathias Charles Joakim (24), mkazi wa Salasala, Kinondoni, na Kassim Abdalah (30), mkazi wa Tegeta — kwa tuhuma za kuvunja nyumba na kuiba fedha taslimu shilingi milioni 105, mali ya mfanyabiashara mwenye asili ya Kichina, Xue Huaxion.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, mara baada ya kupata taarifa za wizi huo Julai 27 mwaka huu, lilifanya uchunguzi na kuwakamata watuhumiwa hawa wawili wakiwa na shilingi milioni 82 na dola za Marekani 267. Fedha zingine walikuwa wamehifadhi kwenye simu zao za mkononi na zingine walizitumia katika miradi ya kufyatua matofali na kununua viwanja,” alisema Muliro.
Kamanda Muliro alisema kuwa uchunguzi utakapokamilika, watuhumiwa wote wawili watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya wizi na uvunjaji nyumba kwa mfanyabiashara huyo mwenye asili ya Kichina.