SIMBA inaendelea kupikwa upya kule Ismailia, Misri, ikipania kutaka kufanya mapinduzi makubwa msimu ujao ikiyataka mataji, lakini watani wao wa jadi, Yanga walikuwa nchini wamejichimbia KMC Complex wakiwa na mipango ya kuwafuata Wekundu hao hukohuko ughaibuni.
Ndio, Yanga imeenda Kigali, Rwanda kwa ajili ya tamasha maalumu litakaloambatana na mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya wenyeji wao, Rayon Sport, kisha itafunga safari hadi katika jiji la kitalii la Alexandria, Misri kuweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya.
Hata hivyo, kama hujui ni kwamba kuna usajili unashtua uliofanywa katika safu za ushambuliaji wa timu hizo unaotoa tahadhari ya mapema kana kwamba wanaambiana ‘Hatutaki lawama’.
Tuanze na Simba, ambao wanafanya mambo yao kwa hesabu kubwa wakitaka kuhakikisha hawarudii makosa ya kugeuzwa wasindikizaji kwa msimu wa tano mfululizo.
Simba hadi sasa ile safu ya ushambuliaji ni kama imekusanya jumla ya mabao 55 fasta kwa aina ya washambuliaji watano waliopo kikosini ambao waliyafunga msimu uliopita wa Ligi Kuu tofauti, wengi wao wakiwa na zaidi ya mabao 10.
Staa wa kwanza wa Wekundu hao katika ufungaji ni Mfungaji Bora Ligi Kuu Bara, Jean Charles Ahoua aliyetikisa nyavu za wapinzani mara 16.
Nyuma ya Ahoua ambaye ni kiungo mshambuliaji kuna washambuliaji wawili, Leonel Ateba na Steven Mukwala ambao kila mmoja amefunga mara 13 katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita.
Lakini katikati yao wamemuongeza Jonathan Sowah ambaye balaa lake ni zito aliyefunga mabao kama hayo akitumia nusu msimu tu, wakati wenzake wakifunga kwa msimu mzima alipokuwa akiitumikia Singida Black Stars, tena akifanya hivyo kupitia duru la pili.
Kasi yake ya kufumania nyavu inashtua na kuonyesha kama angeanza msimu na wenzake, basi pengine ligi ingeshuhudia mfungaji bora tofauti kutokana na kasi yake ya ufungaji.
Wafungaji hao wanne wanaihakikishia Simba mabao wakiwa wamefunga jumla ya mabao 55 kwenye msimu uliopita na sasa wanakwenda kubeba matumaini ya Wekundu wa Msimbazi kwenye kikosi cha kocha Fadlu Davids.
Turudi kwa mabingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA), Yanga, ambao ni kama wanaonyesha hawana hesabu nyingine zaidi ya kutaka kuendeleza mafanikio ya miaka minne kwa kubeba mataji.
Safu ya Yanga katika ushambuliaji itaongozwa na mfungaji wake bora wa msimu uliopita ambaye pia alishika namba mbili katika Ligi Kuu Bara kwa ujumla nyuma ya Ahoua yaani Clement Mzize aliyefunga mabao 14.
Hata hivyo, hesabu mbaya kwa Yanga ni kwamba inataka kumuuza mshambuliaji huyo kinda mara tu baada ya Fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakapomalizika.
Kuondoka kwa Mzize wala haiwapi presha Yanga wakijua wana mtu mwingine kama Pacome Zouzoua ambaye alifunga mabao 13 msimu uliopita, lakini Mwanaspoti linafahamu kuwa mabosi wa klabu hiyo wanapiga hesabu za kushusha mshambuliaji mwingine endapo kinda huyo atauzwa.
Nyuma ya Mzize kuna mfalme mshambuliaji, Prince Dube, aliyefunga mabao 13 sawa na Pacome akiwa kwenye msimu wake wa kwanza ndani ya Yanga akisajiliwa kutoka Azam.
Achana na Dube, Yanga imesajili washambuliaji wawili, wa kwanza ni MVP wa Ligi Kuu Ivory Coast, Celestin Ecua aliyemaliza msimu uliopita akiwa na Asec Mimosas aliyoichezea kwa mkopo kutoka Zoman akifunga mabao 15, na pia wamemuongeza mshambuliaji Andy Boyeli kwenye safu ya ushambuliaji akiwa amefunga mabao sita huko Afrika Kusini akitua kwa mabingwa hao kwa mkopo.
Akizungumzia hesabu za timu hizo mbili, kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alisema Simba inaonyesha kuendelea kutafuta ubora, lakini endapo itawabakisha washambuliaji wote itakuwa na mwendelezo mzuri kwa wanne hao kutaka kuthibitisha ubora wao.
“Tatizo langu Simba ni kama wanaanza upya. Unajua ili uwe na timu bora unayoijenga unahitaji kubakisha msingi wa timu yako. Lakini, sina shaka na washambuliaji sana inategemea timu inayowazunguka hao washambuliaji,” alisema Robertinho aliyetimuliwa Msimbazi mara baada ya Simba kupigwa mabao 5-1 na Yanga katika Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Novemba 5, 2023.
“Kama una washambuliaji waliofunga kuanzia mabao 10 hao sio wachezaji wabovu wanatakiwa kutengenezewa watu ambao watawapa huduma ili wafunge vizuri,” aliongeza kocha huyo Mbrazili.
Kuhusu Yanga, Robertinho alisema bado anaiona inaendelea kusumbua kwa kuwa licha ya kupoteza baadhi ya wachezaji muhimu, lakini ubora wa waliobaki ni mkubwa.
“Yanga bado wanaweza kuendelea kuwa tatizo kwa timu nyingine. Nimeona kuna wachezaji wameondoka kwa kuuzwa hiyo ni biashara ya soka, lakini kwa timu bado ule uti wa mgongo wameubakisha,” alisema Robertinho na kuongeza:
“Safu yao ya ushambuliaji unaona bado ina watu bora tu kama wale wa Simba, lakini kitu hatari ni wale wanaocheza nyuma ya washambuliaji hao ambao ni hatari zaidi. Tusubiri kuona makocha wao watafanya kitu gani.”
Msimu uliopita Yanga ilibeba ubingwa wa Ligi kwa kuitambia Simba mwisho mwa msimu kwa mabao 2-0 baada ya mechi hiyo kupigwa danadana kutoka Machi 8 hadi Juni 15 na kupigwa Juni 25, likiwa ni moja ya mataji matano iliyokomba msimu uliopita, na ikiwa ni mara ya nne mfululizo kubeba taji hilo.
Yanga ilitwaa pia Kombe la FA kwa msimu wa nne mfululizo, Kombe la Muungano na Ngao ya Jamii mbali na Kombe la kimataifa ya Toyota ililotwaa Afrika Kusini, ilihali Simba ilitoka patupu licha ya kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikipoteza mbele ya RS Berkane ya Morocco.