UHONDO wa fainali za Ubingwa wa Nchi za Afrika (CHAN) 2024 unaendelea leo Jumatatu kwa mechi mbili za Kundi C zitakazopigwa jijini Kampala, mapema saa 11:00 jioni Afrika Kusini itajiuliza mbele ya Guinea, ilihali saa 2:00 usiku wenyeji Uganda watakuwa na kibarua kizito mbele ya Niger.
Bafana Bafana iliyoanza michuano hiyo kwa sare ya 1-1 dhidi ya vinara wa kundi hili, Algeria itaikabili Guinea iliyotoka kupoteza mechi iliyopita kwa wenyeji Uganda kwa kukandikwa mabao 3-0, huku wenyeji wakiwa na mzuka wa kutaka kukusanya pointi ili kujiwepa kazuri kutinga robo fainali.
Hadi sasa (kabla ya mechi za jana za Kundi A) ni Tanzania pekee kama wenyeji wa michuano hiyo iliyokuwa imetinga robo fainali ikiwa timu ya kwanza, huku wenyeji wengine Kenya ilikuwa uwanjani jioni ya jana kupepetana na Morocco, ilihali Uganda kibarua chake ni leo kwa Niger.
Fainali za mwaka huu ambao ni za nane tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za ardhi ya nchi husika, imeandaliwa kwa ushirikiano wa nchi tatu wenyeji wa Afrika Mashariki na Tanzania ilitinga robo fainali juzi usiku baada ya kushinda mechi ya tatu mfululizo.
Ushindi huo wa Stars wa mabao 2-1 mbele ya Madagascar umeifanya ifikishe pointi tisa na kuwa timu pekee iliyokuwa imeshinda mechi zote kwa asilimia 100 (kabla ya jana) na kuwa nchi ya kwanza kutangulia robo fainali, huku ikiwa na mechi moja mkononi ya kukamilishia ratiba ya Kundi B.
Tuanze na mechi ya mapema jioni, Guinea iliyoanza na ushindi kabla ya kutulizwa na Uganda ina kazi kubwa mbele ya Bafana Bafana ambao waliiduwaza Algeria kwa kutoka nao sare mechi iliyopita.
Hii ni mechi ya tatu kwa timu hizo kukutana, mara moja ilikutana katika mechi ya makundi ya Afcon 2006 zikiwa Kundi C, ambapo Guinea ilishinda kwa mabao 2-0, lakini 2022 zilikutana katika pambano la kirafiki na kutoka sare ya 1-1.
Hivyo pambano la leo ni la kwanza kwao katika michuano ya CHAN, lakini ni gumu kwa kila mmoja kwa vile kila moja itakuwa inapiga hesabu ya kutoka na ushindi ili kujiweka pazuri katika fainali hizo za nane zitakazofikia tamati Agosti 30.
Guinea itaendelea kuwategemea nyota wake Mohammed Bangoura aliyefunga bao pekee lililoizamisha Niger, mbali na nahodha mwenye jina kama hilo, sambamba na Kabinet Kouyate, Moussa Camara na wengine kuhakikisha wanaisimamisha Afrika Kusini.
Hata hivyo, Guinea inapaswa kukomaa kwani Afrika Kusini sio ya kubezwa ikibebwa na mafundi wa mpira kama Ndabayithethwa Ndlondlo, Thabiso Kutumela, nahodha Neo Maema na wengine katika pambano hilo la pili kwa timu hiyo.
Katika pambano la usiku, Uganda iliyoanza kwa kuchakazwa mabao 3-0 na Algeria kabla ya kuzinduka ikishinda kwa idadi hiyo mbele ya Guinea, itashuka uwanja wa Nelson Mandela, ili kuhakikisha inaendeleza wimbi la ushindi na kujiweka pazuri kuifuta Tanzania hatua ya robo fainali.
Matokeo yoyote kinyume cha ushindi yataiweka pabaya kutokana na ushindani wa kundi hilo linaloongozwa na Algeria, huku itaendelea kuwategemea nyota wake kama Allan Okelo, Reagan Mpande, Ivan Ahimbisibwe na wengine ili kutoka na ushindi mbele ya mashabiki wa The Cranes.
Kwa upande wa Niger ambao hiyo ni mechi ya pili kwao, itakuwa ikihitaji ushindi ili isiendelee kuwa jamvi la wageni kwani ilipoteza mbele ya Guinea katika pambano la kwanza, licha ya bao la utangulizi lililofungwa na Abdoul-Latif Goumey kukataliwa na V.A.R kwa kuonekana mfungaji aliotea.
Hili litakuwa pambano la nane kwa timu hizo kukutana tangu 2008, ikiwamo michezo mitatu ya kirafiki na minne ya mashindano, huku kila moja ikishinda mechi tatu na mmoja kuisha kwa sare.
Mara ya mwisho kukutana ilikuwa mwaka juzi katika pambano la marudiano la makundi ya kuwania fainali za Afcon 2025, ambapo Unagda ilishinda mabao 2-0 baada ya awali kutoka sare ya 1-1, hii ikiwa na maana mechi ya leo ni mechi ya kibabe kwa timu zote na dakika 90 zitaamua mbabe.