Kocha Tanzania Prisons azionya Simba, Yanga

KOCHA Mkuu wa Tanzania Prisons, Zedekiah Otieno amesema licha ya kuwa mara ya kwanza kufundisha soka Tanzania, lakini uwezo na uzoefu alionao katika kazi hiyo itakuwa fursa kwake kujitangaza ndani nje ya Afrika, huku akivionya vigogo, Simba, Yanga na Azam FC.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo raia wa Kenya, alisema kwa muda mrefu amekuwa akitamani kufanya kazi Tanzania kutokana na rekodi iliyopo kwa sasa kwa kuwa na Ligi Bora Afrika na kwamba ujio wake nchini utampaisha zaidi, huku akiahidi makubwa kwa Prisons.

Otieno anatarajia kuiongoza Prisons baada ya msimu uliopita kuifundisha Gor Mahia na tayari ameanza kibarua chake kwa maafande hao jijini Mbeya.

Kocha huyo mwenye Leseni A ya Shirikisho la Soka Afrika, CAF na mkufunzi wa makocha pia nje ya soka ni mhandisi mitambo na mtaalamu wa sanaa ya uchoraji, ambapo katika historia ndio mara ya kwanza kufundisha soka nje ya nchi.

Otieno alisema ilikuwa ndoto yake kufundisha soka nje ya nchi, hivyo fursa aliyopata Tanzania inaenda kumpaisha nje ya Afrika kwa kuwa ushindani na mvuto wa Ligi Kuu kila kocha na mchezaji kwa Afrika anaitamani.

Alisema anachotarajia ni kuona anafanya kazi yake kwa ubora kwa kuipa mafanikio Prisons akieleza kuwa falsafa yake ni muumini wa matokeo ya ushindi na soka la kuvutia kwa mashabiki.

“Cha kwanza mimi nataka matokeo ya ushindi, lakini timu imechezaje, watu wanaokuja uwanjani wanataka burudani, mengine yanafuata,” alisema Otieno na kuongeza;

“Kwa sasa makocha na wachezaji wengi Afrika wanatamani kufanya kazi Tanzania kwa kuwa ligi imekuwa bora, Kenya wengi wanaifuatilia sana na tumekuwa na makocha wengi wakiwamo James Siang’a (marehemu), Francis Baraza, David Ouma na Patrick Odhiambo.”

Kocha huyo aliongeza katika muda wake akishiriki ligi msimu ujao wa 2025/26 hatakuwa na mzaha kwa timu yoyote bali kila mchezo itakuwa vita ya pointi tatu na anahitaji kusaka ushindi wa mechi za mapema na kuomba ushirikiano wa ndani na nje ya uwanja.

“Simba, Yanga na Azam zinajulikana Afrika, lakini niseme kwamba sitakuwa na mzaha wowote kwa timu yoyote, huwezi kukamia mchezo mmoja halafu nyingine uziache, kimsingi nimejipanga na uwezo, nia na uzoefu ninao,” alisema kocha huyo.

Otieno kabla ya kugeukia ukocha, alikuwa mchezaji na beki wa timu kadhaa nchini Kenya ikiwamo Gor Mahia, Sony Sugar na timu ya Taifa ‘Harambee Stars’ akiwa Nahodha kwa timu hizo kabla ya kuzifundisha hadi Prisons ilipomuona.