BEKI mahiri wa zamani wa Singida Black Stars, Yahya Mbegu amedaiwa kujiunga na Mbeya City iliyorejea Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao, akiungana na wachezaji wengine aliowahi kukipiga nao Singida na Mashujaa waliotua katika timu hiyo ya Mbeya.
Beki huyo wa kushoto ambaye msimu uliopita aliitumikia Mashujaa kwa mkopo inadaiwa amesaini mkataba wa mwaka mmoja akiungana na Habib Kyombo, kipa Beno Kakolanya, Jeremie Nkolomoni, Kingu Pemba, Omar Chibada na Ibrahim Ame waliotambulishwa na wababe hao wa jijini Mbeya.
Rafiki wa karibu wa mchezaji huyo aliliambia Mwanaspoti kwamba, mazungumzo ya uongozi wa Mbeya City na beki huyo yamekamilika kwa asilimia kubwa na ameshasaini mkataba wa kuitumikia, kilichobaki ni utambulisho kama uliofanywa wenzake waliotua kikosini hapo.
“Kila kitu kipo sawa, Mbegu msimu ujao atakuwa sehemu ya kikosi cha Mbeya City, ila viongozi wenyewe watatoa ufafanuzi, lakini ni kweli beki huyo ni mali ya Wana Purple,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, hakuna kiongozi wa Mbeya City wala Yahya Mbegu waliopatikana jana kuthibitisha taarifa hizo, japo chanzo hicho kilisisitiza kwamba beki huyo tayari alikuwa njiani kwenda kuungana na wenzake kwa maandalizi ya msimu mpya.
Mbeya City ni kati ya timu mbili zilizopanda Ligi Kuu ikirejea sambamba na Mtibwa Sugar baada ya kufanya vizuri katika Ligi ya Championship ya msimu uliopita kuchukua nafasi za KenGold na Kagera Sugar zilizoshuka.