MSHAMBULIAJI wa Kitanzania, Clara Luvanga ameendelea kukiwasha akiwa na Al Nassr ya Saudia ambayo imeweka kambi huko Hispania kwa maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake.
Huu ni msimu wa tatu wa Clara kuichezea timu hiyo na amekuwa mchezaji tegemeo kikosini akiipa ubingwa mara mbili mfululizo akifunga mabao 32.
Sasa, wakati timu hiyo iko Hispania, juzi ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya PFC Cartama ya nchini humo na Clara alifunga hat-trick katika ushindi wa mabao 7-0.
Achana na hat-trick aliyofunga, kwani amekuwa akifanya hivyo hata katika ligi na mashindano mbalimbali, lakini gumzo ni baada ya mashabiki nchini humo kuandika jina lake kwenye karatasi kubwa.
Katika moja ya matukio yaliyogusa hisia, mashabiki wadogo wawili walionekana wakiwa na mabango yenye majina ya wachezaji wanaowapenda, akiwamo Luvanga.
Picha inaonyesha mvulana mdogo akiwa amebeba bango lililoandikwa jina la Luvanga, namba yake ya jezi 9 pamoja na mchoro wa mpira na bendera ya Tanzania.
Tukio hilo linadhihirisha namna madogo hao wamekubali uwezo na kiwango kilichoonyeshwa na Luvanga.