Dar es Salaam. Katika mwendelezo wa kujenga taasisi bora, bunifu na zenye ushindani na kuchochea ukuaji wa uchumi, Ofisi ya Msajili wa Hazina imepanga kuwakutanisha wakuu wa taasisi na wenyeviti wa bodi 700 za mashirika ya umma nchini ili kupeana mbinu mpya za kuongeza ukusanywaji endelevu wa mapato yasiyokuwa ya kikodi.
Mbali na lengo hilo, wataweka mikakati ya pamoja katika kuboresha utendaji, uwajibikaji na mchango wa mashirika hayo katika uchumi wa Taifa, na kuongeza utawala bora ili kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.
Akizungumza kuhusu mkutano huo unaotarajiwa kufanyika kwa siku tatu, jijini Arusha, kuanzia Agosti 23 hadi 25, 2025, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathimini Mashirika ya Umma, Lightness Mauki amesema sababu ya kuwakutanisha ni changamoto za kiutendaji.
“Pamoja na kwamba tumeanza kuona mafanikio ya kukusanya, Sh1.028 trilioni kwa miaka mitatu, ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita ambapo tulikusanya Sh653 bilioni, lakini tunaona kuna changamoto za kiutendaji na tukiweka nguvu tunaweza kupata kiwango zaidi ya hicho,” amesema.
Lightness amesema Serikali imeweka mtaji wa Sh86 trilion hivyo jitihada zinazochukuliwa ni kutaka tija inayopatikana kuhakikisha inaendana na uwekezaji uliofanywa na Serikali kupitia mashirika hayo.
“Tumejiwekea malengo ya kukusanya Sh2 trillion ni lazima tuziangalie hizo taasisi ili kuzitatua hizo changamoto,” amesema.
Amefafanua wanahitaji kuwa na bodi imara na zinazowajibika kwa kuzingatia teuzi wanazopewa, ziimarike kwa kutambua majukumu yao katika kuongeza ufanisi.
” Kwa mara ya kwanza mkutano huo utajumuisha na taasisi ambazo Serikali ina hisa chache kuanzia moja hadi 50, tunataka kuweka tofauti na mikutano ya miaka mingine ambayo tulikuwa tunaenda taasisi tunazomiliki hisa 100. Tumeona tuzijumuishe kwa sababu ni sehemu ya uwekezaji wa Serikali,” amesema.
“Tunataka kuweka mipango mikakati ya kuongeza makusanyo ya mapato yasiyokuwa ya kikodi pamoja na kwamba tumepiga hatua lakini tunahitaji uwe endelevu na hatuwezi kufikia malengo ikiwa tutakaa ofisini,” amesema Lightness.
Ili kuongeza tija hiyo, Lightness amesema ni lazima wakae pamoja kuoneshana njia ya kufikia shabaha hiyo, na kuona mapato yanakuwa endelevu kwa faida ya Taifa na vizazi vijavyo.
Lightness ametaja mada mbalimbali zitakazojadiliwa katika hizo siku tatu ikiwemo kukuza taaluma zitakazokuwa zinatolewa na wataalamu wabobezi, wawekezaji wa sekta mbalimbali na wataalamu wengine kutoka nje ya nchi.
“Kuna nchi zilizopiga hatua kupitia tija ya mashirika ya umma hivyo tutakuwa na wabobezi kutoka mataifa hayo na wataungana na wataalamu wa ndani katika kujadiliana, na kuja na njia thabiti za kuendeleza taasisi zetu za umma,” amesema
Pia Lightness amesema watakuwa na midahalo ya wazi lakini na maonyesho mbalimbali ya bunifu kubadilisha uzoefu kwa taasisi zilizopiga hatua na kujenga mahusiano ya kitaaluma.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri amesema ni matarajio yao mkutano huo utakuwa na mafanikio.
“Wananchi wafuatilie wajue majukumu ya mashirika ya umma lakini tunaomba vyombo vya habari viendelee kutupa ushirikiano kulitangaza tukio hili muhimu na la kuhabarisha umma,” amesema Kosuri.