Dar es Salaam. Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria, Global Fund umeelekeza Dola za Marekani 544,385,745 sawa na Sh1.35 trilioni kuja Tanzania kwa ajili ya kushughulikia magonjwa hayo kwa miaka mitatu 2024/2026.
Katika kiasi hicho Sh711 bilioni zimeelekezwa kushughulikia afua za VVU/Ukimwi, Sh448 bilioni malaria huku Sh101 bilioni zikitengwa kushughulikia magonjwa ya Kifua Kikuu.
Fedha hizo ni pungufu kwa asilimia 11 na fungu lililotengwa awali, kama bajeti ya Tanzania kushughulikia magonjwa hayo kwa msimu wa saba.
Awali Global Fund ilitenga bajeti ya Dola za Marekani 609,234,336 sawa na Sh1.51 bilioni, hata hivyo hazikufika kwa wakati kutokana na mkwamo wa uwasilishaji fedha katika mfuko huo.
Taarifa ambazo Mwananchi imezipata, kupungua kwa msaada huo kunaondoa shughuli zilizotumia fedha nyingi lakini hazina mantiki zikiwamo vikao, warsha, ununuzi wa magari baadhi ya maeneo, kutokana na mwongozo uliotolewa na Global Fund.
Hata hivyo kama nchi tayari kuna hatua zimechukuliwa kuziba nakisi iliyojitokeza, baada ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2025/2026 kuanzisha vyanzo vya mapato vinane kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya Ukimwi na kugharamia bima ya afya kwa wote.
Kufuatia hilo, Wizara ya Afya imesema kutokana na mabadiliko ya sera za nje kwa wadau mbalimbali, kumekuwa na upungufu wa fedha katika ufadhili sekta mbalimbali, ambapo miradi iliyoathirika zaidi kwenye sekta ya afya ni ya Ukimwi, malaria na Kifua Kikuu.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe amesema ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma bila kikwazo chochote, kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali ilitenga na kutoa Sh141.98 bilioni kwa ajili ya kuhakikisha uendelevu wa huduma.
Amezitaja huduma hizo ikiwemo ununuzi wa dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi (ARVs), malaria na Kifua Kikuu.
“Kwa mwaka 2025/2026, Serikali imetenga Sh158 bilioni kwa ajili kuwezesha upatikanaji huduma za magonjwa haya ikiwemo upatikanaji wa dawa, vitendanishi na vifaa muhimu hadi Juni 2027,” amesema.
Dk Magembe amesema sambamba na kutenga fedha za kununua bidhaa mbalimbali, pia Serikali imeendelea kutoa kibali cha ajira kwa kada mbalimbali za afya ambapo katika kipindi cha kuanzia Julai, 2024 hadi Juni, 2025 imeajiri wataalamu wa afya 13, 564 na kuwapangia vituo vya kazi.
Amesema Serikali itaendelea kutenga fedha kila mwaka wa fedha kulingana na mahitaji yatakavyojitokeza.
Sababu kubwa ya upungufu wa msaada huo ni kutokana na wafadhili kuelekeza fedha nyingi kwenye maeneo mengine, ikiwemo kujitoa kwa USAID Januari mwaka huu ambayo ilikuwa ikichangia asilimia 30 ya mfuko huo.
Mwaka 2023, taarifa iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya Ukimwi (UNAIDS) ilibainisha maeneo hayo kuwa ni pamoja na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Uviko19, homa ya nyani, vita vya Ukraine na majanga mengine, ambayo yalisababisha mdororo wa kiuchumi.
Ripoti imeonyesha nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania bado inasalia kuwa tatizo kubwa, zikichangia idadi kubwa ya maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 59 mwaka 2021. Duniani kote, watu milioni 38.4 walikuwa wakiishi na VVU mwaka 2021 na vifo 650,000 kutokana na magonjwa yanayohusiana na Ukimwi.
Nchi 133 kati ya 195 duniani zipo kwenye hatari ya kukosa rasilimali fedha, huku nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zipatazo 20 zikiwa na hali mbaya zaidi huku wanawake wadogo na wasichana balehe kutoka nchi hizi ripoti imeonyesha wamekuwa waathirika na maambukizi mapya kila baada ya dakika mbili.
Mwaka 2019 Tanzania ilipokea mgao wa Sh1.33 trilioni kutoka Global Fund, ambapo Sh828.19 bilioni zilielekezwa kushughulikia Ukimwi, Sh407.15 bilioni malaria na Sh97.67 bilioni zilikuwa kwa ajili ya ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa kipindi cha mwaka 2020/2022.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania(MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema fedha za mfuko huo zimekuwa zikichangia karibu asilimia 20 mpaka 30 ya bajeti yetu ya sekta ya afya kwa kipindi kirefu.
Amesema hii ni kengele ya kutuamsha kwenye usingizi mzito wa mipango yetu kama nchi, ili bajeti yetu iweze kujitosheleza na kutotegemea wahisani na wadau wa maendeleo.
“Wadau wa maendeleo hatuwakatai wawepo, lakini hawatakiwi waamue mustakabali wa maisha yetu, pale watakapokuwa wamejiondoa Serikali lazima iwe na mikakati ya pamoja na iwaite wadau wote na kujipanga kujitegemea katika sekta ya afya,” amesema Dk Mugisha.
Mratibu wa Kitaifa kutoka COMPASS Tanzania, Francis Luwole amesema athari zitakazotokana na kupungua kwa fungu hilo ni kipaumbele kikubwa kwa sasa, kipo kwenye huduma za kuokoa maisha zaidi zinaangaliwa kama ufuatilizi na matibabu.
Amesema huduma za kijamii kama elimu, kuboresha mifumo ya afya hazitakuwa kipaumbele kikubwa kutoka katika mfuko huo, hivyo inakwenda kupungua.
“Sasa ukiangalia kwenye VVU na Ukimwi maambukizi mapya ni 60,000 ikitokea fedha zikapungua katika eneo la udhibiti maambukizi mapya tutegemee maambukizi kuongezeka ndani ya miaka michache ijayo, Serikali itaingia hasara tena kununua dawa na kutibu,” amesema.
Luwole amesema jambo la msingi ni kubadilisha vipaumbele, kama nchi tuangalie tulivyokuwa navyo awali, kwa kuyapa kipaumbele mambo yenye matokeo makubwa kwa kutumia fedha ndogo.
Amesema ili kuokoa gharama muhimu kuunganisha huduma zinazoendana, kwani mwelekeo wa ulimwengu kwa sasa fedha za ufadhili zitaendelea kupungua, ni muda muafaka kutunisha mifuko ya kushughulikia magonjwa kwa fedha za ndani.
“Tunaweka vipaumbele kwenye huduma zipi na tusipuuze huduma za kijamii, kinga za kuokoa maisha. Ni vitu vya kuzingatiwa VVU peke yake inachukua fedha nyingi, kwa miaka mingi tumekuwa tukitegemea ufadhili kwenye eneo hili kwa asilimia 90,” amesema Luwole.
Mkurugenzi wa Shirika la Dare, Dk Lilian Mwakyosi amesema katika mzunguko huu wa saba ambao ulishaanza Januari Mosi 2024, Mei mwaka huu iligundulika tayari rasilimali zilikuwa chache na fungu limepungua kwa zaidi ya asilimia 11, hivyo ni muda wa nchi kuendelea kujipanga.
“Kwenye afua za virusi vya Ukimwi, malaria na TB imepungua kwa asilimia 11 na hatujui itafananaje tunapoingia mzunguko wa nane mwaka 2027/2029,” amesema.
Juni 12, mwaka huu akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali 2025/2026 Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alisema hatua hizo zimefuatia mabadiliko ya kisera yanayoendelea duniani, ambayo yamesababisha wadau muhimu wa maendeleo kupunguza misaada iliyokuwa inatolewa kwa ajili ya huduma za afya, ikiwemo kukabiliana na kudhibiti magonjwa mbalimbali hususan Ukimwi.
Alisema Serikali inapendekeza kuanzisha vyanzo mbadala vya mapato, ili kupunguza nakisi ya kibajeti iliyotokana na kupungua kwa misaada hiyo kwa kufanya marekebisho katika sheria mbalimbali.
“Inapendekezwa asilimia 70 ya mapato yatakayoongezeka ipelekwe kwenye Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) na asilimia 30 ipelekwe kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote,” alisema.
Pamoja na kiasi hicho cha fedha iliyoelekezwa moja kwa moja kushughulikia magonjwa hayo, pia mfuko huo umelipatia Shirika la MDH Dola za Marekani 36.97 milioni sawa na Sh91.7 bilioni.
Awali Global Fund ilielekeza Dola za Marekani 41 milioni kwa shirika hilo, ambayo ni sawa na Sh101.7 bilioni.