BAADA ya danadana za muda mrefu juu ya dili la mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize kuuzwa nje ya nchini, hatimaye mabosi wa klabu hiyo wameridhia kutua Esperance ya Tunisia na kuelezwa sababu ya kuchomolewa kwa ofa ya klabu ya Umm Salal ya Qatar.
Awali mchezaji huyo alihusishwa na klabu kutoka Ubelgiji, Misri, Afrika Kusini na Morocco kabla ya juzi kati kuibuka taarifa ya ofa hiyo kutoka Qatar, mbali na ile ya Al Masry ya Misri.
Hata hivyo, taarifa ni kwamba mabosi wa Yanga wamekubali ofa ya Esperance ya kumnunua straika huyo tegemeo wa timu ya taifa, Taifa Stars na kuweka bayana sababua ya kuichomolea klabu ya Qatar iliyokuwa imetangulia mapema kumtaka mchezaji huyo.
Chipukizi huyo mwenye kipaji aliyepanda haraka viwango akiwa na Yanga, alivutia klabu hivyo vikubwa vya Uarabuni, ambapo kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka Yanga ni Umm Salal ilitoa ofa ya Dola za Marekani 900,000 (Sh2.2 bilioni) pamoja na mshahara wa Dola 20,000 (Sh50 milioni) kwa mwezi kwa mchezaji huyo.
Katika makaratasi, kifurushi hicho cha kifedha kilionekana kikubwa, lakini mabosi wa Yanga umesema pesa pekee siyo kigezo cha uamuzi wa kumtoa mchezaji huyo.
Mmoja wa vigogo wa klabu hiyo aliyezungumza na Mwanaspoti, amesema sababu kuu ya kukataa ofa ya Umm Salal ni hadhi na ushindani wa klabu hiyo ya Qatar.
“Umm Salal sio klabu kubwa Qatar na msimu uliopita ilimaliza ligi ikiwa nafasi za chini,” alisema kigogo huyo aliyeombwa kuhifadhiwa jina aliyeongeza;
“Kwa mchezaji kijana kama Mzize, ambaye ana uwezo mkubwa, tunaamini ni muhimu ajiunge na klabu kubwa barani au angalau timu ya kiwango cha kati huko Ulaya.”
Yanga imehofia kwenda Umm Salal kunaweza kuzuia maendeleo ya Mzize kwa kumweka katika mazingira yasiyo na ushindani wa kutosha.
“Kumruhusu Mzize aende Umm Salal ni kuhatarisha kipaji chake,” alisisitiza ofisa huyo na kuongeza; “Tunataka aende kwenye klabu ambayo itamlazimisha kupigania nafasi yake, kuonyesha uwezo wake na kukua kwenye mazingira yenye ushindani.”
Kwa upande mwingine, Mwanaspoti limefanikiwa kuona barua ya Esperance waliyoiandikia uongozi wa Yanga juu ya kuwa tayari kutoa ofa ya Dola 1 Milioni (Sh2.6 milioni), ikiwa imetimiza masharti yote yaliyoweka na mabosi wa Jangwani.
Mabingwa hao wa Tunisia walitoa ofa ya Dola 1 Milioni, ikiwa ni angalau zaidi ya Umm Salal, pia walikuja na hadhi ya moja ya klabu zinazofanya vizuri zaidi Afrika.
Esperance ni mabingwa mara nne wa Ligi ya Mabingwa Afrika na msimu uliopita ilishinda taji la 34 la Ligi ya Tunisia ikithibitisha ubabe katika soka la Afrika Kaskazini, pia ilikuwa miongoni mwa klabu zilizocheza Fainali ya Kombe la Dunia kwa Klabu 2025 zilizofanyika Marekani.
“Kwa kiwango, Esperance ni miongoni mwa timu kubwa zaidi barani, sambamba na Zamalek wa Misri na vigogo kama Wydad Casablanca,” chanzo hicho cha Yanga kimesisitiza.
“Tuna historia ya kufanya biashara na vilabu vya hadhi hiyo, kumbuka dili letu na Wydad kwa Stephane Aziz Ki. Esperance wanafaa kabisa kwenye kundi hilo.”
Kwa Yanga, uamuzi huu haukuwa tu kuhusu ada ya uhamisho wa papo hapo, bali pia faida za muda mrefu za kisoka kwa mchezaji na klabu.