KOCHA wa Harambee Stars, Benny McCarthy ameitaja Tanzania kuwa mojawapo ya timu zinazoshiriki dimba la CHAN 2024 ambazo zina hamu ya kuifunga Kenya.
McCarthy alinukuliwa akisema: “Kazi kubwa yetu ya kumaliza mechi za makundi inayofuata ni dhidi ya Zambia. Naweza kusema kwa kujiamini kuwa timu zote kwenye michuano hii zinafanya juhudi kubwa kuifunga Kenya miongoni mwa timu hizo ni Tanzania,” akasema mkufunzi huyo.
Alikumbusha matamshi yake ya kitambo aliyowahi kuyasema kuwa Kenya itakuwa timu hatari zaidi nchi yoyote na hilo limethibitika katika mashindano haya yanayoendelea nchi za Kenya, Tanzania na Uganda.
“Kenya ilionekana kuwa timu dhaifu zaidi katika kundi A na wengi walidhania iutamaliza nafasi ya mwisho katika kundi hilo. Hata hivyo, tuliwaangusha DRC waliopigiwa upatu kushinda dimba hilo, wakaja Angola, tukacheza nao na watu 10 kwa zaidi ya dakika 70 na tukaenda sare.
“Tulikutana na Morocco, wababe wa soka barani Afrika na kama ilivyokuwa, tulipata nyekundu dakika ya 41 ya kipindi cha kwanza, tukacheza watu 10 tena kwa zaidi ya dakika 50 na bado tukaweza kuwanyamazisha,” akasema McCarthy.
Baadhi ya mashabiki wa soka wa Kenya wamepokea maongezi ya baadhi ya wafuasi wa Taifa Stars kutaka wapangiwe Harambee Stars.
“Hata sisi tuna hamu kubwa ya kupambana na Taifa Stars tuwaonyeshe cha mtema kuni,” amesema mkurugenzi wa ufundi wa Cosmos FC Aref Baghazally.
“Nimeona maoni ya mashabiki wa Taifa Stars wakitamba kuitaka Harambee Stars kwenye mechi za maondoano. Yataka mashabiki wa Tanzania waelewe kuwa sisi ndio tuko kwenye kundi gumu zaidi na tunaomba tukutane nao kuamuliwe nani bora kati yetu na wao,” akasema Baghazally.
Mkufunzi huyo ambaye amepewa ruhusa kuchagua kikosi chake bila ya kuingiliwa amesema atakuwa akishuhudia mechi kadhaa za ligi za hapa nchini mbali na kutaka Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) limpe fursa ya kwenda ng’ambo kuangalia jinsi Wakenya wanavyocheza huko.
“Nia kubwa ni kutaka kila mchezaji mwenye kustahili kuwa kikosi cha timu ya taifa apate kucheza kuonyesha ubora wake. Nataka kwenda Uhispania na Ulaya kuona jinsi wanasoka Wakenya wanavyosakata soka huko,” akasema.
Alisema anataka wachezaji wa ng’ambo watambuwe kuwa hakuwasahau kwa michuano mingine ya kimataifa.
“Nitawachagua wale walio bora kuweka kwenye kikosi cha Harambee Stars kitakachoshiriki mechi ambazo zinaruhusu wanasoka wa ndani na nje kushiriki,” akasema McCarthy.