Wataalamu wapewa mafunzo usahihi wa maudhui ya akili unde

Dar es Salaam. Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kwa kushirikiana na Wakala wa Usalama wa Mtandao Korea Kusini (KISA) wanaendesha mafunzo ya usalama wa mtandao kwa Watanzania 33 kuanzia leo Jumatatu Agosti 11 hadi 15, 2025 jijini Dar es Salaam.

Mafunzo hayo ni kwa ajili ya kuongeza wataalamu wa usalama wa mtandao kwenye taasisi mbalimbali za Serikali na sekta binafsi, kuongeza imani ya watumiaji pamoja na kuangalia matatizo ya usalama wa mtandaoni katika zama hizi za akili unde.

Akizungumza nje ya mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Dk Nkundwe Mwasaga amesema ili watu watumie fursa zitokanazo na uchumi wa kidijitali inabidi imani ya mifumo iwepo kwa watumiaji.

“Ili mtumiaji awe na imani mifumo inapaswa kuwa salama kuanzia taarifa binafsi, ulinzi wa faragha, kumlinda mlaji wa mifumo ya kidijitali. Mafunzo haya ya siku tano tutaangazia mambo hayo yote.

Akitolea mfano nchi ya Korea Kusini amesema imedhamiria kuwa na wataalamu wa usalama wa mtandao wapatao 10,000 wenye uwezo wa ulinzi wa mitandao ya kidijitali.

Amesema ujuzi wanaoupata watu hao 33 wataenda kuwapatia na wenzao, akisema pia sasa hivi wahalifu wana mbinu mbalimbali zinazobadilika kila siku, kwa hiyo usalama wa mtandaoni unahitaji pia mafunzo ya mambo mapya kila wakati.

“Sisi pia, tuna mikakati tumejiwekea ikiwemo uchumi wa kidijitali, dira ya 2050, yote haya yanahitaji kuwa na wataalamu wengi kama wahalifu walivyokuwa nao wengi ili kuwa na uchumi wa kidijitali kuongeza wawekezaji, watu kuwa huru kutumia mitandao yenye fursa mbalimbali.”

Akirejea mafanikio ya Tanzania kutajwa kuwa kundi la kwanza la nchi zaidi ya 40 zenye usalama bora kama ilivyoainishwa na Tasisi ya Umoja wa Mataifa (ITU), amesema Serikali imenuia kuhakikisha inapata wataalamu wengi haraka iwezekanavyo.

“Sasa hivi huduma nyingi zinafanyikia mtandaoni, maisha ya watu wengi wanategemea mifumo, malipo, huduma mbalimbali za kiserikali, kwa hiyo wataalamu wanahitajika kila wilaya, tarafa na sehemu zote bila kusahau elimu kwa wananchi,” amesema.

Mtafiti kutoka KISA, Minyoung Kim amesema ni muhimu kwenda na wakati ukirejea Mapinduzi ya AI yaliyopo duniani hivyo mafunzo kama hayo yatasaidia wataalamu wa Kitanzania, huku akiahidi kuendeleza ushirikiano.

Miongoni mwa washiriki, Venance Mwanjabike kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kitengo cha Tehama, amesema kukua kwa matumizi ya akili unde ikiwemo teknolojia za Deepfake kunahitaji uchunguzi wa kitaalamu.

“Jinsi ya kujua video hii imetengenezwa ama haijatengenezwa na akili unde ni changamoto inayohitaji ujuzi wa kitaalamu pamoja na vifaa ikiwemo software. Tunahitaji kuongeza wataalamu pamoja na mafunzo kama haya,” amesema.

Naye, Ester Foi kutoka Tume ya Tehama amesema wataalamu wanapaswa kujua mambo mengi ikiwemo jinsi ya kupata ushahidi wa taarifa kutoka kwenye mitandao.

 “Tunajifunza vitu ikiwemo kupata ukweli kuhusu video, picha na sauti zinazozalishwa na akili unde,” amesema.