Kesi ya kuporomoka jengo Kariakoo yafikisha siku 255, upelelezi bado

Dar es Salaam. Kesi ya kuua bila kukusudia inayowakabili wafanyabiashara sita wakiwemo wamiliki wa jengo lililoporomoka Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo imefikisha siku 255 bila upelelezi kukamilika.

Hata hivyo, upande wa mashtaka umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa bado unaendelea na uchunguzi katika kesi.

Washtakiwa katika kesi hiyo ambao wote ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ni Leondela Mdete (49) mkazi wa Mbezi Beach, Zenabu Islam(61) mkazi wa Kariakoo na Ashour Awadh Ashour(38) mkazi wa Ilala.

Wengine ni Soster Nziku(55) mkazi wa Mbezi Beach, Aloyce Sangawe(59) mkazi wa Sinza na Stephen Nziku(28) mkazi wa Mbezi Beach.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Novemba 29, 2024 na kusomewa mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia katika kesi ya mauaji namba 33633/2024.

Tangu siku hiyo hadi leo Jumatatu Agosti 11, 2025, kesi hiyo imefikisha siku 255 ambazo ni sawa na wiki 36 na siku tatu, bila upelelezi kukamilika.

Hata hivyo, washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.

Leo, kesi hiyo ilipoitwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini kwa ajili ya kutajwa,  Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele amesema kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

“Mheshimiwa hakimu, washtakiwa wote wapo mbele ya Mahakama yako na kesi hii imeitwa leo kwa ajili ya kutajwa, lakini upelelezi wake bado unaendelea, hivyo tunaomba mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa” amesema Roida

Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maelezo hayo, alikubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 11, 2025.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa yao kinyume na kifungu 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022

Kwa pamoja wanadaiwa Novemba 16, 2024 katika Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, washtakiwa hao isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha kifo cha Said Juma.

Katika shtaka la pili hadi la 31, washtakiwa hao siku na eneo hilo wanadaiwa kusababisha vifo vya watu zaidi ya 30 wakiwamo Hussein Njou, Prosper Mwasanjobe, Shadrack Mshingo, Godfrey Sanga, Neema Sanga, Elizabeth Mbaruku, Hilary Minja, Abdul Sululu na Catherine Mbilinyi.

Pia Elton Ndyamukama, Mariam Kapekekepe, Elizabeth Kapekele, Hadija Simba, Frank Maziku, Rashid Yusuph, Ally Ally, Ajuae Lyambiro, Mary Lema na Khatolo Juma.

Wengine ni Sabas Swai, Pascal Ndunguru, Brighette Mbembela, Ashery Sanga, Venance Aman, Linus Hasara, Pascalia Kadiri, Issa Issa, Lulu Sanga, Happyness Malya na Brown Kadovera.