Tanzania yaanza kujipanga uzalishaji umeme kwa nyuklia

Dar es Salaam. Mpango wa Tanzania kutumia nyuklia kama chanzo cha nishati umeanza, baada ya kusaka teknolojia ya kuzalisha umeme kwa nishati hiyo bila kusababisha madhara.

Hatua hiyo inakuja wakati Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (Taec) imeingia makubaliano ya kushirikiana na Shirika la Global Center for Nuclear Energy Partnership la nchini India.

Makubaliano haya yatawezesha ufadhili wa masomo kwa vijana wa Tanzania kushirikia kwenye utafiti na kuendeleza mafunzo na teknolojia zitakazowezesha matumizi salama ya nishati hiyo katika uzalishaji wa umeme.

Akizungumza leo Jumatatu Agosti 11, 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Taec, Profesa Najat Mohammed amesema Tanzania na India zimekuwa na ushirikiano wa undugu, hivyo makubaliano hayo yatasaidia katika matumizi salama ya nishati ya nyuklia.

“Kupitia makubaliano haya, tutaendeleza matumizi salama ya nyuklia, sasa teknolojia inakua kwa haraka, hivyo tutaangalia namna ya kutumia, tuwe na usalama wa chakula, pia kuzalisha umeme na kuitumia hasa ikizingatia nchi yetu imeonesha nia ya kuelekea huko,” amesema.

Balozi wa Tanzania nchini India, Bishwadip Dey amesema Tanzania na India zimekuwa na ushirikiano kwa muda mrefu, hivyo ujuzi uliopo baina ya mataifa hayo utatumika kuwanufaisha wananchi.

“Tumekuwa na ushirikiano na Tanzania katika sekta ya afya, elimu na maeneo mengine mengi, ushirikiano huu utakuwa na matunda, tutatoa ufadhili wa masomo na kusaidia namna ya kulinda nyuklia itumike salama na isiwe na madhara kwa wananchi,” amesema.

Utekelezaji huo unakuja ikiwa ni miezi mitatu imepita tangu Mei 25, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange alipoagizwa na Rais Samia Suluhu Hassan, asimamie mradi wa uzalishaji wa umeme wa nyuklia kwa kutumia madini ya uranium yanayopatikana Tunduru mkoani Ruvuma.

Rais Samia alitoa maagizo hayo jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua, akiwamo mkurugenzi huyo.

Rais Samia alisema kwa muda mrefu nchi imekuwa na madini hayo, lakini hayajatumika kama chanzo cha uzalishaji wa umeme.

“Kwa makadirio ya sasa hivi, ni takribani tani 58,500 za uranium zimelala pale, nadhani wakianza kuchimba na kufanya ugunduzi kwenye eneo lile wanaweza kupata mengi zaidi,” alisema Rais Samia.

 “Huu mradi uanze, umeme wa nyuklia kama wao wanautumia, tunaweza kuutumia, tukawa na umeme wa kutosha nchini na kuuza nchi jirani kama tunavyotaka kuuza sasa kwa Zambia,” alisisitiza.

Kwa Mujibu wa Wizara ya Nishati, mahitaji ya umeme nchini kwa sasa yanakua kwa asilimia 10 hadi 15 kwa mwaka na ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu, Tanzania imepanga kuzalisha megawati 10,000 za umeme ifikapo mwaka 2030, hivyo kuanza kwa uzalishaji huo ni hatua ya kufikia malengo hayo.

Katika kuendeleza na kutumia nishati ya nyuklia nchini, inatiliwa mkazo Sera ya Nishati ya mwaka 2015, Sera ya Madini ya mwaka 2009, Mpango Kamambe wa Kuendeleza Sekta ya Umeme na Mkakati wa Nishati Jadidifu.