CCM kufanya harambee ya kuchangisha mabilioni ya fedha

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema Kamati Kuu ya chama hicho imeamua kufanya harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kukiandaa kuelekea kampeni za Uchaguzi Mkuu zitakazoanza Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025.

Amesema mchango wa fedha katika harambee ya chama hicho hauwezi kuwa kigezo cha kupata uteuzi kwa makada wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi.

CCM inalenga kukusanya Sh100 bilioni kupitia harambee hiyo, huku ikieleza fedha hizo zitatumika katika maandalizi ya kampeni za uchaguzi mkuu.

Dk Nchimbi amesema hayo leo Jumatatu, Agosti 11, 2025 katika mkutano wake na wahariri, waandishi uliofanyika ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.

Amesema harambee hiyo itafanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam kuanzia saa 11 jioni na mgeni rasmi atakuwa Mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Dk Nchimbi amesema kwa sasa CCM ina wanachama zaidi ya 13.19 milioni waliosajiliwa kidijitali.

Amesema kampeni zinahitaji rasilimali fedha pamoja na magari, mabango na vitu vingine hivyo wameamua kufungua milango kwa yeyote vikiwemo vyama vya upinzani kama wanataka kuwachangia na wafanye hivyo.

Amesema kila mwanachama anaruhusiwa kuchangia bila kujali kama ni mgombea au la, lakini hakuna atakayeteuliwa kwa sababu ya kiasi cha fedha alichotoa.

“Hakuna mtu atakayeteuliwa kwa sababu alichangia Sh20 bilioni. Kamati za maadili zimeshakaa na kupitia tabia za wagombea. Hatuiti kikao cha maadili cha dharura kwa sababu mtu ametoa mamilioni,” amesema Dk Nchimbi, alipojibu swali harambee hiyo haitatumiwa na watiania ambao mchakato wa uteuzi unaendelea kushawishi kamati za uteuzi.

Ameongeza heshima ya chama haiwezi kuuzwa, na hakuna mtu anayeweza kununua uteuzi kupitia mchango wake, lakini wanachama wote wanahimizwa kushiriki kuchangia.

Kuhusu watu kutumia fursa hiyo kutoa fedha kwa malengo yao, Dk Nchimbi amesema hakitakubali kupokea mchango wowote unaoweza kudhalilisha heshima na uhuru wa Tanzania katika harambee hiyo.

Amesema michango yote itakayopokelewa itachunguzwa chanzo chake kabla ya kukubaliwa.

“Tutaangalia inatoka wapi. Ile inayodhalilisha heshima au kupoteza uhuru wa nchi yetu hatutaipokea. Hatuwezi kupokea michango inayopoteza utu wa Watanzania,” amesisitiza Dk Nchimbi.