Mwanza. Kituo cha Kuratibu, Utafutaji na Uokoaji (MRCC) kinachojengwa jijini Mwanza kinatarajiwa kukamilika mwezi ujao kikitajwa kuwa uti wa mgongo wa usalama wa majini.
Kituo hicho kikuu cha kuratibu shughuli za uokoaji, utafutaji na usalama wa majini katika Ziwa Victoria, kikishirikiana na vituo vidogo vinavyopatikana katika miji mikubwa na bandari kama Bukoba, Kemondo, Kisumu (Kenya), Entebbe na Jinja vya Uganda, ambavyo vitasaidia kutoa huduma za uokoaji haraka katika nchi zinazozunguka na ziwa hilo.
Kwa sasa kimekamilika kwa asilimia 95 ikiwa ni sehemu ya mradi wa Kimataifa wa Mawasiliano na Usafirishaji wa Majini katika Ziwa Victoria (MLVMCT), unaoratibiwa na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), kwa ushirikiano wa Serikali za Tanzania na Uganda.

Katibu Mkuu wa Wizara inayoshughulikia Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Uganda, Edith Mwaje
Akizungumza wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara inayoshughulikia Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Uganda, Edith Mwaje, pamoja na ujumbe wake katika kituo hicho, Katibu Mkuu wa LVBC, Masinde Bwire amesema mradi huo wa kikanda umebuniwa ili kuboresha usafiri wa majini, kuongeza usalama wa usafiri huo, na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na dharura.
Dk Bwire ameongeza kuwa mradi huo unagharimu zaidi ya dola za Marekani 1.87 milioni, ambapo Serikali za Tanzania na Uganda kwa kushirikiana na kamisheni hiyo zinahakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati.

Katibu Mkuu wa LVBC, Dk Masinde Bwire akizungumza wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara inayoshughulikia Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Uganda, Edith Mwaje ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Kikanda cha Kuratibu, Utafutaji na Uokoaji (MRCC) ndani ya Ziwa Victoria
“Serikali ya Uganda imetoa asilimia 100 ya fedha zake kwa ajili ya ujenzi na sasa inasubiri ankara za vifaa vya majini ili kulipa sehemu yake husika. Serikali ya Tanzania itakamilisha malipo ya mwisho kwa mkandarasi na washauri mara nyaraka zitakapokamilishwa, jambo linalotarajiwa kufanyika Septemba 2025,” amesema Dk Bwire.
Amefafanua kuwa kituo cha MRCC kimeundwa kwa kuzingatia mikataba ya kimataifa iliyowekwa na Shirika la Kimataifa la Usafirishaji wa Majini (IMO) na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), kitakachofanya kazi kila siku ndani ya saa 24.
Amesema, kituo hicho kitatumikia kuratibu shughuli za utafutaji na uokoaji majini, kushughulikia taarifa za dharura na kutoa taarifa kwa wahusika, kuratibu maeneo ya utafutaji na rasilimali za msaada, pamoja na matibabu ya dharura na uokoaji wa wagonjwa.

Katibu Mkuu wa Wizara inayoshughulikia Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Uganda, Edith Mwaje akikagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Kikanda cha Kuratibu, Utafutaji na Uokoaji (MRCC) ndani ya Ziwa Victoria kinachojengwa jijini Mwanza
Pia, kitashughulikia kufuatilia usalama wa usafirishaji wa majini, kufanya mafunzo ya waokoaji, na kudumisha utayari wa kiutendaji kwa ajili ya misheni za uokoaji.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara inayoshughulikia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Uganda, Edith Mwaje amesema jumuiya hiyo itahakikisha mradi unakamilika kwa wakati ili kuwa na kituo imara cha utafutaji, ufuatiliaji, na uokoaji kwa masilahi ya wavuvi na watumiaji wa Ziwa Victoria katika nchi wanachama.
Mwaje ameongeza kuwa wavuvi na wasafirishaji ndani ya ukanda wa Ziwa Victoria wana haki ya kulindwa wakati wote, jambo ambalo jumuiya imeipa kipaumbele kwa kujenga kituo maalumu pamoja na kuweka boti za kisasa za uokozi, ufuatiliaji, na huduma za matibabu ndani ya ziwa hilo.
Mkurugenzi wa Huduma za Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), Hamidu Mbegu amesema mradi huo ni wa kikanda, lakini Tanzania kwa kuonyesha kuthamini mchango wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, imetoa eneo lenye ukubwa wa hekari 3.5 mkoani Mwanza kwa ajili ya utekelezaji wake.
“Mradi huu unaleta mabadiliko makubwa katika kushughulikia utafutaji na uokoaji, kwani ajali nyingi zimekuwa zikitokea, lakini uratibu wa uokoaji haukuwa mzuri. Kwa jitihada za pamoja, lazima tushirikiane ili kuboresha huduma,” amesema Mbegu.
Awali, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Balandya Elikana amesema Serikali ya Tanzania ni mnufaika mkubwa wa mradi huo kwani utasaidia kuwalinda wavuvi na kukamata majangili ndani ya Ziwa Victoria.
Ameongeza kuwa Serikali imejiandaa kupokea matunda chanya ya mradi huo, kwani ndani ya Ziwa Victoria kuna miradi ya uvuvi, kama vile boti za kisasa zilizotolewa kwa wavuvi kwa mkopo, ambazo zinazingatia viwango vya kimataifa vya uhifadhi wa mazingira.

Katibu Mkuu wa LVBC, Dk Masinde Bwire akizungumza wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara inayoshughulikia Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Uganda, Edith Mwaje ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Kikanda cha Kuratibu, Utafutaji na Uokoaji (MRCC) ndani ya Ziwa Victoria
Historia ya ajali Ziwa Victoria
Ziwa hilo ambalo ni kubwa zaidi barani Afrika na la pili kwa ukubwa duniani kwa maji ya juu ya ardhi limekuwa eneo la ajali nyingi za meli na boti, hasa kutokana na hali ya hewa ya ghafla, uchakavu wa vyombo vya usafiri, na ukosefu wa usalama wa ziwani.
Baadhi ya ajali ambazo zimetokea katika Ziwa Victoria ni ajali ya MV Nyerere (Tanzania) iliyotokea Septemba 20, 2018. Ajali hiyo ilitokea jirani na Kisiwa cha Ukara, Mwanza na kusababisha vifo takribani watu 228 huku sababu ikielezwa kuzidisha abiria.
Ajali nyingine ilitokea Mei 21, 1996 ambapo meli ya MV Bukoba ilizama kwenye eneo kati ya Mwanza na Bukoba, ambapo ilisababisha vifo vya zaidi ya watu 800, huku sababu ikitajwa ni kuzidisha abiria kupita kiwango, na haikuwa na vifaa vya kutosha vya usalama.
Pia, Desemba 21, 2020 upande wa Kenya ilitokea ajali ya boti kwenye eneo la Mbita, Kaunti ya Homa Bay na kusababisha vifo vya takribani watu 17 huku sababu ikitajwa ni boti hiyo ya uvuvi kuzidisha abiria na mizigo, na hali ya hewa ilikuwa mbaya.
Nchini Uganda kati ya mwaka 2020 na 2021 zimetokea ajali kadhaa za boti za wavuvi huku kila moja ikisababisha vifo vya kati ya watu watano hadi 20 huku sababu zikielezwa kutumia boti zisizo salama, bila vifaa vya kujiokoa.