MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inatarajia kukutana na Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) ili kujadili na kufafanua kwa uwazi nani anastahili kutambulika kama mwanablogu nchini.
Hatua hiyo inafuatia malalamiko ya TBN kwamba wanablogu wa kitaaluma wamekuwa wakichanganywa na watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaomiliki akaunti binafsi au za kibiashara, lakini hawana blogu rasmi zenye maudhui ya kitaalamu na muundo maalumu.
Kwa mujibu wa Meneja wa Huduma za Utangazaji wa TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka, kikao hicho kinatarajiwa kuondoa mkanganyiko uliopo kati ya wanablogu na watengenezaji wa maudhui wengine wa mtandaoni. Amesema maafisa wa TCRA watajadili hoja za TBN, kupitia mfumo wa kisheria uliopo, na kuangalia uwezekano wa marekebisho yatakayozingatia ukuaji wa vyombo vya habari vya mtandaoni nchini.
Mhandisi Kisaka alitoa kauli hiyo wakati wa mafunzo ya wanachama wa TBN kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, yaliyofanyika katika makao makuu ya TCRA jijini Dar es Salaam, kutekeleza agizo la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, amesema anaamini kuwa kupitia makubaliano ya pamoja, wanachama wa mtandao huo watapata utambuzi rasmi na nafasi thabiti ya kushiriki katika mijadala ya sera za kidijitali nchini.
Hatua hii inakuja wakati tasnia ya maudhui ya kidijitali ikikua kwa kasi, huku ushawishi wa mitandao ya kijamii, vlogu na tovuti za habari mtandaoni mara nyingi ukifanana, jambo linalofifisha mipaka ya maana halisi ya mwanablogu katika zama hizi za uchumi wa kidijitali.