Dodoma. Serikali imeombwa kutoa elimu zaidi ya usimamizi wa miradi ya mazingira ili kusaidia Taifa kuondokana na jangwa, ukame.
Wito huo umetolewa leo Jumatatu Agosti 11,2026 na Mratibu wa Mradi wa Taifa wa Forland, Emma Nzunda katika kilele cha maonyesho ya wakulima Nanenane katika viwanja vya maonyesho Nzuguni Jijini Dodoma.
Mradi huo mpya wa Forland unajihusisha na Misitu na Matumizi ya Ardhi na Maendeleo ya Mnyororo wa Thamani unaofadhiliwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Tanzania na Finland kutokana na mafanikio ya Mpango Shirikishi wa Upandaji Misitu (PFP2) na Mpango wa Kukuza Misitu na Thamani (FORVAC).
Matarajio ya mradi huo ni uboreshaji wa usimamizi wa misitu ya wakulima wadogo, kuongezea taasisi za kielimu, kuimarisha uhusiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma ili kuboresha sera ya misitu.
“Tuko hapa Nanenane kutambulisha Forland ili wananchi wengi zaidi waufahamu na uwasaidie mwananchi mmojammoja katika uhifadhi wa misitu na matumizi bora ya ardhi,” amesema Zunda.
Amesema Forland inafungamana kwa karibu na vipaumbele vya maendeleo vya Serikali ya Finland na Tanzania na inachangia katika kupunguza umaskini, kuzalisha ajira na kuimarisha ustahimilivu wa hali ya hewa.
Miongoni mwa matokeo muhimu yanayotarajiwa kutokana na mradi huo ni uboreshaji wa usimamizi wa mashamba ya miti ya wakulima, uimarishaji wa kitaasisi katika elimu ya misitu, kuongezeka kwa mazungumzo kati ya wadau wa umma na binafsi ili kuboresha mazingira ya sera ya misitu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Misitu na Viwanda vya Misitu (FWITC), Bertha Nyodewa amesema kituo hicho kinafanya kazi kwa karibu na Forland ili kuwapa wakulima maarifa na utaalamu zaidi.
Nyodewa amesema wanahitaji kuongeza uelewa kuhusu miche bora, usimamizi endelevu wa misitu, mipango ya matumizi mazuri ya ardhi na jinsi upandaji miti unavyoweza kuwa biashara yenye faida,” amesema.
Mjumbe wa Chama cha Wakulima wa Miti Tanzania (TTGAU), Kastory Timbula, ameeleza kufurahishwa kwake na mradi huo ambao umewaongezea wakulima maarifa kuhusiana na kilimo hicho.