Uganda yaendelea kugawa dozi, ikiizima Niger

TIMU  ya taifa ya Uganda The Cranes, imeendelea kung’ara katika michuano ya CHAN 2024 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Niger ikiwa ni mechi yao ya tatu ya Kundi C iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, jijini Kampala.

Uganda ilianza michuano hiyo kwa kipigo cha mabao 3-0 kutoka Algeria, lakini imezinduka mbele ya Guinea iliyoilaza 3-0 kabla ya kuizima Niger 2-0, matokeo yaliyoiweka kileleni mwa kundi hilo.

Katika mechi hiyo, The Cranes ilitawala sehemu kubwa ya mechi, hasa kipindi cha kwanza ambapo ilimiliki mpira kwa asilimia 57 na kuizuia Niger kuingia kwenye eneo lao la hatari. Presha hiyo ilizaa matunda dakika ya 25 wakati Uganda ilipopewa penalti.

Allan Okello, kiungo mshambuliaji wa Uganda, alipiga penalti hiyo lakini kipa wa Niger, Tanja alitema hata hivyo, Okello alimalizia na kuwaweka wenyeji hao mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ile ile, huku Uganda ikionekana kutafuta bao la pili mapema. Ndoto yao ilitimia dakika ya 57, Joel Sserunjogi alipachika bao la pili na kuihakikishia ushindi Uganda.

Uganda inaongoza kundi hilo kwa pointi sita, huku Algeria ikishika nafasi ya pili na pointi nne sawa na Afrika Kusini zote zikicheza mechi mbili, Guinea ina pointi tatu na Niger ikiburuza mkia ikiwa haina pointi kutikana na kupoteza  mechi mbili za awali

Kwa matokeo haya, Uganda sasa inasubiri mechi ya  mwisho dhidi ya Afrika Kusini, huku ikiwa na tumaini la kutunga robo fainali ya mashindano hayo yanayoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani.