Mbinu za kuchopeka mahiri za maisha kwenye  mtalaa wa elimumsingi

Mtalaa ulioboreshwa nchini Tanzania (2023), pamoja na mambo mengine, unalenga kuwajengea wanafunzi mahiri za maisha zinazowawezesha kumudu changamoto za karne ya 21.

Mahiri hizi, ambazo wakati mwingine hufahamika kama stadi za maisha, aghalabu hazionekani moja kwa moja kwenye mtaala na hivyo huhitaji mwalimu awe na uwezo wa kutafuta namna ya kuzikuza wakati somo lake likiendelea.

Kwa mujibu wa mtalaa ulioandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) mahiri hizi ni kama vile fikra tunduizi na udadisi; kujitambua, ushirikeli na ushirikiano; ubunifu, utatuzi wa matatizo na uvumbuzi lakini pia kujitegemea, uongozi na uzalendo.

Tunaweza pia kutaja mahiri nyingine kama vile ujumuishi, usawa wa kijinsia, uvumilivu na ustahamivu, utunzaji wa mazingira na maadili.

Mahiri hizi ni muhimu kwa sababu zinawasaidia wanafunzi kufanikiwa katika jamii inayobadilika kwa kasi, kukuza uelewa wa kibinafsi na kijamii, na kuwatayarisha kwa changamoto za kiuchumi, kijamii, na kiutamaduni wakati na baada ya masomo yao.

Kwa mfano, fikra tunduizi huwasaidia kufanya uamuzi wa busara, huku uzalendo ukimjenga mwanafunzi kujitambulisha vyema na mila zake, desturi za jamii yake na utamaduni.

Hata hivyo, changamoto kubwa imekuwa ni jinsi ya kuzifundisha mahiri hizi wakati somo la kawaida linaendelea.

Badala ya kuhitaji vipindi vya ziada, mwalimu anaweza kuzichopeka kupitia shughuli za ujifunzaji zinazolingana na somo lake, huku wanafunzi wakijijengea mahiri hizi wakati mwingine bila wao kujua wanajifunza mahiri hizi. Makala haya yanalenga kupitia mahiri hizo na kujadili mbinu zinazoweza kutumika kuzikuza na kuzipima.

Fikra tunduizi ni uwezo wa mwanafunzi kufikiri kwa kina, kuchanganua taarifa, na kufanya uamuzi unaoongozwa na uchambuzi wa taarifa alizonazo. Kinyume na fikra tunduizi ni kukariri na kurudia rudia yale yale aliyofundishwa na mwalimu wake.

Fikra tunduizi hujitokeza pale mwanafunzi anapohoji dhana, kulinganisha mawazo, au kutoa tathmini ya kimantiki badala ya kuishia kukumbuka taarifa alizokutana nazo.

Katika somo la kemia, kwa mfano, mwalimu anaweza kuwapa wanafunzi shughuli ya kuchanganua tofauti ya milinganyo ya kikemia ambayo kwa kawaida, wanafunzi huishia kuikariri. Badala ya ‘kuwamezesha’ milinganyo, mwalimu anawauliza, mathalani, sababu hasa ya kile wanachokiona kama matokeo ya mlingano wake.

Katika somo la Kiswahili, hili pia linawezekana. Badala ya kuwapa dondoo za namna ya kuandika barua, mwalimu anaweza kuwapa mifano ya barua mbili zilizokosewa uandishi na kuwataka wanafunzi wafanye ulinganisho kulingana na matini waliyojifunza. Shughuli hii inawachochea kuhusisha taarifa na kufikiri kwa kina.

Mwalimu anaweza kutathmini fikra tunduizi kwa ripoti za majaribio au majibu ya mdomo, akizingatia mantiki ya hoja, ushahidi, na uchanganuzi wa mwanafunzi.

Udadisi ni hamu ya mwanafunzi kujifunza zaidi na kuuliza maswali. Kinyume cha udadisi ni kuridhika na majibu mepesi, wakati mwingine, yasiyokidhi shauku ya kujifunza.

Udadisi unajitokeza mwanafunzi anapochunguza mada mpya, kutafuta majibu, au kushiriki katika utafiti, kama vile kuuliza kuhusu asili ya jamii fulani.

Katika somo la maarifa ya jamii, kwa mfano, mwalimu anaweza kuwapa wanafunzi mradi wa kuchunguza “Kwa nini jamii za Wamasai zilihama?” Shughuli hii haiwalazimishi wanafunzi kwenda umasaini, bali kutafuta vyanzo vya kihistoria, kama vitabu au maongezi na wazee, na kuandika ripoti fupi.

Mwalimu anaweza kuwapa maswali  chokozi au ongozi, kama, “Je, mazingira yalichangia vipi?” Shughuli hii ikifanyika vyema inawachochea kuuliza maswali ya kina.

Ushirikiano ni uwezo wa mwanafunzi kufanya kazi na wengine kwa pamoja akilenga kufikia lengo la wengi. Huwezi kuwa na ushirikiano bila kutambua lengo kuu linalowaunganisha na wenzako. Kinyume cha ushirikiano ni ubinafsi. Ushirikiano hujitokeza mwanafunzi anaposhiriki katika kazi za kikundi, kushirikiana mawazo, au kutatua migogoro.

Katika somo la fizikia, kwa mfano, mwalimu anaweza kugawa wanafunzi katika vikundi vya watu wanne kufanya jaribio la kupima nguvu ya msuguano kwenye nyuso tofauti.

 Kila mwanafunzi atakuwa na jukumu lake (mfano kupima, kuandika, kuongoza), na kisha watajadili jinsi ya kuboresha jaribio. Mwalimu anaweza kuwauliza waandike ripoti ya kikundi.

Ushirikeli ni uwezo wa kuelewa na kujali hisia za wengine. Ushirikeli ni zaidi ya huruma kwa mwenzako na hujitokeza mwanafunzi anapojali wenzake au kushiriki katika shughuli za kijamii, kama vile kusaidia katika masuala ya afya ya jamii.

Katika somo la biolojia, mwalimu anaweza kuandaa mchezo wa kuigiza kuhusu jinsi ya kusaidia jamii inayokabiliwa na ugonjwa wa malaria.

Wanafunzi wataigiza majukumu ya wataalamu wa afya au wanajamii, wakiwasilisha suluhu zinazojali wengine. Mwalimu anaweza kuwauliza wajadili jinsi hisia za wanajamii zinavyoathiriwa. Shughuli hii inakuza ushirikeli kwa kuwafanya wanafunzi wazingatie wengine.

Kujitambua ni uwezo wa mwanafunzi kubaini na kuelewa nguvu, udhaifu, na malengo yake. Wengine huchukulia kujitambua kama sehemu ya umahirihisia unaojitokeza pale mwanafunzi anapofikiri namna uamuzi wake unavyoathiri wengine na hivyo kuchochea kujirekebisha.

Katika somo la kemia, mwalimu anaweza kuwapa wanafunzi shughuli ya kutafakari baada ya jaribio la kutengeneza kimiminika cha kemikali. Wanafunzi wataandika “Je, wapi nilifanya vizuri? Wapi naweza kuboresha zaidi?” na kuweka malengo ya kuboresha majaribio yao ya baadaye.

Ubunifu ni uwezo wa kutoa mawazo mapya yasiyotarajiwa. Unapokuwa mbunifu maana yake hutegemei unachokijua na mazoea na ndio maana ubunifu hujitokeza mwanafunzi anapounda kitu cha kipekee, kama vile kukokotoa jibu la kihisabati kwa njia yake mweyewe.

Katika somo la hisabati, kwa mfano, mwalimu anaweza kuwapa wanafunzi kazi ya kuunda muundo wa kijiometri (mfano tetrahedron) kwa kutumia vifaa kama vijiti au karatasi. Wanafunzi wataunda miundo tofauti na kuelezea jinsi inavyohusiana na dhana za kijiometri.

Shughuli hii inawachochea kufikiri nje ya mazoea.Mwalimu anaweza kutathmini ubora wa miundo na maelezo yao, akizingatia uhalisi na uhusiano na dhana za hisabati.

Utatuzi wa matatizo ni uwezo wa kufikiri na kupata majibu ya changamoto halisi. Kinyume cha utatuzi wa matatizo ni kuendekeza nadharia zisizo na uhusiano wa moja kwa moja na changamoto za kila siku.

Mahiri hii hujitokeza mwanafunzi anaposhughulikia maswali magumu au miradi, kwa kutumia visa mafunzo, matukio halisi au hata mafumbo,

Katika somo la jiografia, mwalimu anaweza kuwapa wanafunzi mfano wa tatizo: “Kijiji kimeathiriwa na ukame. Gawanya rasilimali za maji kwa jamii ya watu 100.” Wanafunzi watajadili njia za kugawanya maji kwa usawa na kuhalalisha suluhu zao.

Mwalimu anaweza kuwapa ramani ya kijiji kama zana ya kujifunzia. Shughuli hii ikifanyika vizuri inakuza ujuzi wa kutatua matatizo.
Mwalimu anaweza kutathmini suluhu zilizotolewa kwa usahihi, mantiki, na uwezo wa kushirikiana.

Uvumbuzi ni uwezo wa kutumia mawazo mapya katika kuboresha hali ya mambo. Uvumbuzi ni tofauti na ugunduzi ambapo mtu huja na kitu ambacho aghalabu hakijawahi kuwepo. Mwanafunzi mwenye uvumbuzi anaweza kuunganisha taarifa alizonazo na kuja na majibu yanayoboresha jambo au namna tunavyochukulia jambo.

Katika somo la Kiswahili, mwalimu anaweza kuwapa wanafunzi kazi ya kutunga tamthilia fupi inayohusisha suluhu za changamoto za kijamii, kama umaskini.

 Wanafunzi wataandika na kuigiza tamthilia inayoonyesha jinsi mhusika anavyovumbua njia ya kutoka kwenye umaskini. Shughuli hii inakuza uvumbuzi kwa vitendo.Mwalimu anaweza kutathmini tamthiliya kwa uhalisi, utendakazi wa suluhu na ubora wa uwasilishaji.

Uongozi ni uwezo wa kuwashawishi wengine kufikia maono fulani. Kiongozi, kwa kawaida, ni muonaji anayewafanya wengine waone kile anachokiona, na kuwawezesha kufikia maono hayo. Uongozi unajitokeza pale mwanafunzi anapojiamini, kuona anaweza kusema mawazo yake na kuwashawishi wenzake kukubaliana na mtazamo wake.

Katika somo la fizikia, kwa mfano, mwalimu anaweza kugawa wanafunzi katika vikundi vya kuandaa wasilisho kuhusu nishati mbadala, kama umeme wa jua. Kila kikundi kitachagua kiongozi atakayesimamia mgawanyo wa kazi na kuongoza majadiliano.

Mwalimu anaweza kutoa mwongozo wa maswali ya wasilisho. Shughuli hii inakuza uongozi wa pamoja.Mwalimu anaweza kuchunguza uwezo wa kiongozi kusimamia kikundi, ushirikiano wake na ubora wa wasilisho.

Uzalendo ni tabia ya kujitambulisha na desturi zake, mila zake na tamaduni za jamii yake. Uzalendo, tofauti na uchawa, hujitokeza pale mwanafunzi anapoweka mbele maslahi ya jamii yake na kuthamini utamaduni na asilia yake.

Katika somo la biolojia, kwa mfano, mwalimu anaweza kuwapa wanafunzi mradi wa kuchunguza mimea ya asili ya Tanzania na jinsi jamii za asili zinavyotumia mimea hiyo katika dawa za jadi. Hili linaweza kufanyika katika kila somo, kwa kuhakikisha kuwa mwanafunzi, mara zote, anatazamishwa thamani ya asili yake.

Kwa msingi huo wanafunzi watawasilisha ripoti inayohusisha uthamini uliopo katika tamaduni za Tanzania. Shughuli hii inakuza uzalendo kupitia uelewa wa urithi wa kitamaduni. Mwalimu anaweza kutathmini ripoti au wasilisho, akizingatia uelewa wa mwanafunzi wa tamaduni na mazingira ya Tanzania.

Nimalizie kuwa mwalimu anaweza kuchopeka mahiri hizi bila kuhitaji kipindi kinachojitegemea. Kupitia shughuli za ujifunzaji zinazolingana na masomo ya kawaida, kama majaribio ya kemia, miradi ya maarifa ya jamii, kazi za kikundi za fizikia, michezo ya kuigiza ya Kiswahili, mwalimu anaweza kuwasaidia wanafunzi kujijengea mahiri hizi kwa njia ya asili na hivyo kuwaandaa wanafunzi kwa changamoto za karne ya 21 bila kubadilisha muundo wa darasa.

Mwandishi ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, mtafiti wa elimu ya hisia katika ujifunzaji na mshauri mwelekezi katika masuala ya ujifunzaji. Unaweza kuwasiliana naye kwa 0746944444