KATIKA kuhakikisha inajiandaa na msimu mpya wa Ligi ya Wanawake, inaelezwa Yanga Princess imewaongezea mikataba wachezaji wawili kuendelea nao msimu ujao.
Mabeki hao ni Diana Mnally na rafiki yake wa karibu Protasia Mbunda, waliokuwa wamejiunga na Yanga Princess msimu uliopita wakitokea Gets Program.
Inaelezwa nyota hao walionyesha kiwango bora msimu uliopita, hali iliyowashawishi viongozi wa wananchi kuwaongezea mikataba ya kuendelea nao.
Chanzo kiliiambia Mwanaspoti kuwa tayari wameongeza mikataba, na msimu huu Yanga haitawaacha wachezaji waliofanya vizuri msimu uliopita, kwani malengo ni kufanya vizuri na kutwaa ubingwa wa ligi.
“Wachezaji muhimu wote wameongezewa mikataba, na mipango ya Yanga msimu ujao ni kushindana na kunyakua taji la ligi. Wanaongeza wachezaji katika baadhi ya maeneo, lakini hawatawaacha wale waliofanya vizuri ambao mikataba yao ilikuwa inaisha,” kilisema chanzo hicho.
Mbali na mabeki hao wazawa, inaelezwa pia Yanga imewaongezea mikataba kiungo mshambuliaji Aregash Kalsa raia wa Ethiopia, straika Jeaninne Mukandayisenga na kiungo Adebis Ameerat.