Simba yamvizia kiungo wa Stars

KAMA ulidhania Simba imefumba jicho la usajili basi umekosea, licha ya kwenda Misri kujiandaa kwa msimu mpya wa mashindano ya msimu ujao wa 2025-26, lakini mabosi wa klabu hiyo wanaendelea kusaka vyuma na sasa inadaiwa wametua KMC wakitaka kiungo mkabaji aliyepo Taifa Stars.

Simba imeweka kambi katika jijini la Ismailia ikiwa inaingia wiki ya pili sasa, ambako kocha Fadlu Davids akiendelea kuwasoma wachezaji wapya na wale waliokuwa msimu uliopita, lakini akiwa pia anaendelea kupiga hesabu za kuongeza mashine nyingine kuzidi kujiimarisha.

Mwanaspoti linafahamu kuwa, Simba sasa imeanza kumpigia hesabu kiungo Ahmed Bakari ‘Pipino’ ambaye ni miongoni mwa wachezaji wanaochipukia kwa kasi Ligi Kuu Bara kwa kiwango bora alichokionyesha msimu uliomalizika aliyepo timu ya taifa, Taifa Stars katika fainali za CHAN.

Unaweza usilisikie sana jina lake, ila kazi yake uwanjani imewavutia mabosi wa Simba ili kile ambacho amekionyesha KMC na Stars, ikiwezekana akakifanye pia Msimbazi msimu ujao.

Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa, ni kweli mchezaji huyo amepigiwa simu na kocha wa Simba akimwambia kwamba anamhitaji katika kikosi hicho kilichomaliza nafasi ya pili ya Ligi Kuu na kukata tiketi ya ushiriki wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayoanza mwezi ujao.

“Tuko kwenye mazungumzo na Simba, kocha ndiye aliyempigia mchezaji baada ya kuvutiwa na kiwango chake, hivyo kama tutafikia makubaliano muda ukifika tutaweka wazi,” mmoja ya watu wanaomsimamia mchezaji huyo alisema.

Hata hivyo,  Mkurugenzi Mtendaji wa KMC, Daniel Mwakasungula alipotafutwa na Mwanaspoti alisema, hawana taarifa yoyote kuhusu Pipino kutakiwa na Simba, ila wanachofahamu ni kwamba yuko kwenye majukumu ya timu ya taifa.

“Simba haijafika kwetu, hivyo hakuna taarifa yoyote kutoka kwetu kuhusu kutakiwa kwa Pipino, ninachojua yuko katika jukumu la kuitumikia Taifa Stars na anatuwakilisha vyema,” alisema Mwakasungula.

Katika nafasi anayoichezea Pipino, Simba yuko Yusuf Kagoma, ambaye yuko kikosi kimoja cha Stars katika mashindano ya CHAN yanayoendelea.

Licha ya kwamba Pipino ana mkataba wa miaka miwili na KMC, lakini ana nafasi ya kusajiliwa na Simba kwa sababu nafasi ya kuongeza wachezaji wazawa bado ipo.

Katika nafasi hiyo Simba tayari imemsajili Msenegal Alassane Kante, akiwa kama mrithi wa Fabrice Ngoma ambaye aliondoka baada msimu uliopita kumalizika.