-Utoro wapungua; Ufaulu waimarika
Na Mwandishi Wetu – Uyui
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), wameendeleza juhudi kubwa za kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi Wilayani Uyui, mkoani Tabora, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuinua ubora wa elimu nchini.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano maalum yaliyosainiwa kati ya TEA na UNICEF, yenye lengo la kuboresha miundombinu ya elimu katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Songwe. Kupitia ushirikiano huo, jumla ya miradi 48 ya elimu inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya mikoa hiyo.
Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, miradi minne tayari imekamilika, ikiwa na thamani ya takriban shilingi milioni 162.8. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa matundu 10 ya vyoo katika Shule ya Sekondari Nsololo, pamoja na ukarabati na umaliziaji wa maabara nne za masomo ya sayansi katika shule za sekondari za Goweko, Usagari na Kizengi.
Utekelezaji wa miradi hiyo umekuwa chachu ya maboresho makubwa katika mazingira ya kujifunzia, na hivyo kuchochea ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi mmoja mmoja pamoja na maendeleo ya kitaaluma katika shule kwa ujumla.
Mazingira bora, ufaulu waimarika
Mkuu wa Shule ya Sekondari Nsololo, Mwalimu Paulina Mereka, alisema kabla ya utekelezaji wa mradi huo, shule ilikuwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya vyoo.
“Shule yetu ina wanafunzi 500 lakini tulikuwa na matundu manne tu ya vyoo, yaliyotumiwa na wanafunzi na walimu. Hali hii ilikuwa changamoto hasa kwa wanafunzi wa kike, na kwa kweli iliathiri mahudhurio na utulivu wa ujifunzaji,” alisema Mwl. Mereka.
Aliongeza kuwa, ujenzi wa matundu 10 ya vyoo umekuwa mkombozi mkubwa kwa shule hiyo na umeleta matumaini mapya katika ukuaji wa taaluma.
“Sasa tuna uhakika wa ongezeko la mahudhurio, mazingira salama ya kujifunzia, na pia ufundishaji utaimarika. Tunaamini hali hii itaongeza ufaulu wa kitaaluma shuleni,” alisisitiza.
TEA na UNICEF wanaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ya elimu ili kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kujifunza katika mazingira bora, salama na rafiki kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kusimamia upatikanaji wa elimu bora na kwa usawa kote nchini.
Muonekano wa nje wa maabara ya Sayansi Shule ya Sekondari Goweko iliyopo Wilayani Uyui, Mkoani Tabora.