Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo, Dar es Salaam leo inatarajiwa kutoa uamuzi wa shauri la maombi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kuhusiana na mashahidi wa Jamhuri katika kesi inayomkabili ya kuchapisha taarifa za uwongo mtandaoni, kutoa ushahidi bila kuonekana.
Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa na Jaji Elizabeth Mkwizu kufuatia shauri la maombi ya mapitio ya Mahakama alilolifungua Lissu.
Katika shauri hilo anapinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu, iliyoamuru mashahidi wa Jamhuri katika kesi hiyo ambao ni raia watoe ushahidi wao bila kuonekana na kutokutajwa majina yao wala taarifa zao zinazoweza kufanya wakatambulika.
Badala yake anaiomba mahakama hiyo itengue uamuzi huo wa mahakama ya chini ili mashahidi hao watoe ushahidi wao katika hali ya kawaida, yaani wafike mahakamani na kutoa ushahidi wao hadharani, wakionekana.
Lissu anakabiliwa na kesi ya kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa Youtube, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, katika Mahakama ya Kisutu, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.
Kabla ya kuanza kwa usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka, Jamhuri (Serikali) ilifungua shauri dogo la maombi ya ulinzi wa mashahidi wake ambao ni raia (wasio askari Polisi).
Katika shauri hilo, Jamhuri iliomba mashahidi hao watoe ushahidi wao kwa kificho yaani bila kuonekana mahakamani, wala majina yao na taarifa zao zinazoweka kufanya wakatambulika, wao binafsi, familia zao na mahali wanakoweza kupatikana.
Jamhuri ilifungua shauri hilo kwa madai kuwa mashahidi hao wamekuwa wakipata vitisho kutoka kwa watu wa karibu na mshtakiwa huyo, ili wasiende Mahakama kutoa ushahidi.
Taarifa hizo zilielezwa pia katika viapo vilivyounga mkono maombi hayo, kiapo cha Wakili wa Serikali Tawabu Issa na cha Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu, Dar es Salaam (ZCO) Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Faustine Mafwele.
Shauri hilo lilisikilizwa upande mmoja wa Jamhuri, kama Sheria inavyoelekeza na Hakimu Mhini katika uamuzi wake alioutoa Juni 9, 2025, alikubaliana na hoja na maombi hayo ya Jamhuri, akatoa amri hizo kama zilivyoombwa na Jamhuri.
Lissu hakukubaliana na uamuzi huo, hivyo Juni 25, 2025, alifungua Mahakama Kuu shauri hilo la maombi ya mapitio ya Mahakama, akiiomba mahakama hiyo iitishe jalada la kesi yake kuchunguza mwenendo na uamuzi huo kujiridhisha na uhalali na usahihi wake na hatimaye iutengue.
Shauri hilo lilisikilizwa na Jaji Mkwizu, Julai 16, 2025, ama Lissu kupitia jopo la mawakili wake alibainisha na kufafanua kwa kina sababu kupinga uamuzi huo.
Hata hivyo, sababu na hoja hizo zikipingwa na Jopo la mawakili wa Serikali lilipinga sababu hizo kuwa hazina mashiko, huku nao wakitoa ufafanuzi wa kina.
Kwa iwapo Mahakama Kuu itakubaliana na hoja zake, basi inaweza kutengua uamuzi huo na kwa hiyo mashahidi hao watatoa ushahidi wao hadharani ambapo naye Lissu hataweza kuwaona na kuwatambua.
Pamoja na mambo mengine jopo la mawakili wa Lissu lilidai kuwa hapakuwa na sababu za msingi zilizotolewa kuifanya Mahakama ya chini kutoa uamuzi huo.
Mmoja wa mawakili wa Lissu, Dk Rugemeleza Nshala alidai kuwa viapo vya hao mashahidi ambao walidai kuwa walitishiwa vilipaswa viwepo ili Hakimu aweze kutoa uamuzi wa haki, lakini hakuna viapo walivyoviwasilisha mahakamani kama ushahidi wa madai hayo.
Wakili Jebra Kambole alidai kuwa katika uamuzi ule hakimu hakufanya uchambuzi wa kiwango cha upande wa mashtaka kuthibitisha madai yao kwa kiwango kinachotakiwa, yaani bila kuacha mashaka na kwamba angefanya uchambuzi sawasawa asingeamua hivyo.
Alidai kuwa uamuzi huo uliathiri haki za mshtakiwa za usikilizwaji sawa, kwani Mahakama haipati fursa ya kumtathimini shahidi kuaminika kwake wakati akitoa ushahidi kizimbani wala mshtakiwa kupata fursa ya kumkabili ana kwa ana.
Kwa upande wake Wakili Jeremiah Mtobesya alidai kuwa sababu zilizotolewa haziwezi kuondoa umuhimu wa Mahakama kuangalia mwenendo wa nje wa shahidi wakati akitoa ushahidi kizimbani (demeanor).
Akijibu hoja hizo kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali, Wakili wa Serikali Kuu, Nassoro Katuga, kwanza aliomba Mahakama itupilie mbali maombi ya Lissu.
Alihoji iwapo kifungu 372 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kilichotumika kufungua shauri hilo kinaipa mahakama hiyo mamlaka kulisikiliza.
Alifafanua kuwa uamuzi wa Mahakama ya Kisutu unaolalamikiwa, ulitolewa kwa mujibu wa sheria na kwamba Mahakama ilijikita katika ushahidi wa viapo viwili vilivyotolewa Wakili wa Serikali ZCO, ACP Mafwele.
Wakili Katuga alidai kiapo cha Mafwele, kilieleza kuwa amepokea taarifa fiche kuwa kuna mashahidi ambao sio polisi kuwa wamekuwa wakipokea vitisho vya kutoa ushahidi katika kesi hizo.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema pamoja na mambo mengine aliiomba hiyo isiingie kwenye mtego kwa kupelekwa maombi hayo ya mapitio, akidai kuwa yana sura ya rufaa.
Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu. Katika mashtaka hayo Lissu anadaiwa kumhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutenguliwa kwa wagombea chama chake katika maeneo mbalimbali wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, 2024.
Pia, anadaiwa kuwatuhumu askari Polisi kuhusika katika wizi wa kura kupitia vibegi na majaji kutokutenda haki kwa madai ya kutaka wapate uteuzi wa Rais kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani.
Anadaiwa kutenda makosa hayo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai umma.
Katika hatua nyingine, askari polisi watano na raia watatu wanaokabiliwa na mashtaka 16 ya kughushi vibali vya kumiliki silaha, pamoja na askari Polisi mwingine anayekabiliwa na kesi ya kumiliki bastola na risasi 26 bila kibali, Mkaguzi wa Polisi (Insp.) Fredrick Malekela(45), watafikishwa tena mahakamani hapo leo.
Maofisa hao wa Polisi wanaotuhumiwa kughushi vibali hivyo ni Mkaguzi wa Polisi Fredrick Malekela (45), Sajenti Kalemwa Kaunga (54), Sajenti Edger Mlogo (54), Sajenti Robert Titus (47) na Sajenti John Kaposwe (46).
Washtakiwa wenzao ambao ni raia ni mkulima Damson Mnyilenga (59), wafanyabiashara Simon Aloyce (60) na Venrand Liberio(29).
Kesi hizo ambazo zote mbili zinasikilizwa na Hakimu Mhini, leo zinakuja kwa ajili ya kutajwa.