CAF yaiadhibu Kenya, yapunguza mashabiki Moi Kasarani

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limetoa adhabu ya kupunguzwa kwa idadi ya mashabiki katika Uwanja wa Moi Kasarani uliopo Nairobi, Kenya kutokana na kujirudia kwa matukio ya vurugu yanayovunja kanuni za ulinzi na usalama viwanjani katika fainali za CHAN 2024 zinazoendelea.

Barua ambayo CAF imeandika kwa mwenyekiti wa Kamati ya Ndani ya maandalizi (LOC) ya Kenya imeijulisha nchi hiyo kuwa kuanzia sasa, Uwanja wa Moi Kasarani utakuwa unaingiza asilimia 60 tu ambayo ni sawa na mashabiki 27,000 ambayo ni tofauti na idadi kamili ya mashabiki ambayo Uwanja huo inaweza kuhimili ambao ni 48,000.

CAF imeanika sababu za kuchukua uamuzi huo ambazo imesema kuwa ni uvunjwaji wa kanuni za ulinzi na usalama za shirikisho hilo.

“Licha ya maonyo na adhabu kadhaa, hatua muhimu za kudhibiti mashabiki wasio na tiketi, kuhakikisha kuna usimamizi wa umati wa watu na kukidhi matakwa ya ulinzi ya CAF, hazijachukuliwa.

“Udhaifu mkubwa wa kiusalama unajumuisha kuruka mageti ya uwanja kwa mashabiki wasio na tiketi, kushindwa udhibiti wa awali wa mashabiki uliopelekea uingiaji usio rasmi kwenye baadhi ya mageti, matumizi ya mabomu ya machozi.

“Matukio hatarishi kama urushaji wa mawe kwa maofisa usalama, kutokuwepo na polisi wa kutosha licha ya maombi ya usaidizi wao, kutokuwepo kwa ripoti ya matibabu kufuatia ripoti ta majeruhi na vifaa vichache vya mawasiliano na kamera za CCTV katika maeneo nyeti ya kuingilia,” imefafanua barua hiyo ya CAF.

Kutokana na hilo, CAF imetoa adhabu tatu ambazo ni kuruhusu mashabiki 27,000 tu kuingia uwanjani hapo sawa na asilimia 60, kuhitaji mashabiki wenye tiketi za kielektroniki tu kuingia uwanjani na tatu ni kuitaka serikali ya Kenya na kamati yake ya maandalizi ya mashindano hayo kuonyesha uwajibikaji mbele za umma na  kuanzisha kampeni za vyombo vya habari ili kutoa elimu kwa mashabiki kufuata protokali za kiusalama.

Mbali na adhabu hizo, CAF imetoa onyo kali kwa Kenya kwamba inaweza kutafuta viwanja mbadala iwapo hayo iliyoagiza hayatofanyiwa kazi au makosa yaliyojitokeza yatarudiwa tena.