UCHAMBUZI WA MJEMA: Tatizo la ajira kete ya kisiasa, ACT-Wazalendo kuzizalisha milioni 12

Moshi. Ni dhahiri tatizo la ajira nchini, limegeuka kete ya kisiasa katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani 2025 ambapo chama cha ACT-Wazalendo, kupitia ilani yake ya uchaguzi (2025-2030) kimeahidi kuzalisha ajira milioni 12.

Hii ni tofauti na Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho katika ilani yake ya uchaguzi, kimeahidi kuzalisha ajira zenye tija zisizopungua milioni 8, katika sekta rasmi na isiyo rasmi na nusu ya ajira hizo zitazalishwa katika sekta rasmi nchini.

Wasomi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii wanasema kuzalisha ajira hizo inawezekana, lakini kinachopaswa kutazamwa ni njia gani zinazotumika kuzizalisha hasa kwa vijana, ikizingatiwa ni bomu linalosubiri kulipuka.

Hata hivyo, Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma katika Chuo Kikuu cha St Augustino cha Tanzania, Dk Kaanael Kaale alisema maendeleo ya sayansi na teknolojia yanaweza kuathiri baadhi ya nafasi za ajira.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Conrad Kabewa, alienda mbali na kusema kutaja namba za idadi ya ajira zitakazozalishwa haitoshi, bali ni aina gani ya ajira ndio suala la msingi. Alisema  kiongozi hapaswi kujivunia bodaboda kama ajira.

Ripoti ya Ajira Rasmi na Kipato (Tanzania Formal Sector Employment and Earnings survey) iliyotolewa Julai 2025 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inaonyesha Tanzania Bara na Zanzibar, ina wafanyakazi 4,073,887 walioko katika ajira rasmi.

Sekta binafsi ndio  waajiri wakuu nchini ikiwa imeajiri wafanyakazi 2,853,566 katika sekta rasmi ikilinganishwa na watumishi 1,220,322 katika sekta ya umma.

Lakini takwimu za tovuti ya TICGL Data Driven Centre inaonyesha  hapa nchini sekta isiyo rasmi inaongoza katika nyanja ya ajira ikiwa na asilimia 71.8 ya wafanyakazi, au takriban wafanyakazi milioni 25.95 wakijihusisha na kazi zisizo rasmi.

Tatizo la ajira kwa vijana ni la kidunia, takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO), zinaonyesha kiwango cha ukosefu wa ajira kwa mwaka 2023 kilikuwa asilimia 5.1, lakini kwa Tanzania viwango vinatofautiana kulingana na chanzo cha habari.

Kwa mujibu wa Macrotrends, kiwango cha ukosefu wa ajira nchini Tanzania kwa mwaka 2023 kilikuwa asilimia 2.58 kikipungua kwa asilimia 0.01 ya mwaka 2022.

ACT Wazalendo na ajira milioni 12

Chama cha ACT-Wazalendo, kupitia ilani yake ya uchaguzi mkuu 2025, imeainisha vipaumbe saba ambapo  cha kwanza kinahusu ahadi ya uchumi wa watu utakaozalisha ajira rasmi milioni 12 katika kipindi cha miaka mitano.

“Tunalenga kujenga uchumi wa watu kwa kuzalisha ajira milioni 12 kupitia viwanda, kilimo, uvuvi, mifugo, biashara ndogo ndogo, sanaa, teknolojia na huduma za Kijamii,”inaeleza ilani hiyo iliyozinduliwa wiki iliyopita jijini Dar.

“Serikali ya ACT Wazalendo (iwapo watafanikiwa kuongoza dola) itajihusisha kikamilifu katika shughuli za kiuchumi kwa kufanya uwekezaji wa kiwango kikubwa katika maeneo ya uzalishaji na kuwezesha wananchi kuwa injini ya uchumi wa Taifa,”inaeleza ilani hiyo ya ACT Wazalendo.

ACT Wazalendo wanasema kwa Taifa kuwa na uchumi imara, unaokua na endelevu ni lazima uchumi huo utokane na watu wenyewe kupitia shughuli zao za kilimo, uvuvi, ufugaji, viwanda, utalii, biashara na biashara ndogondogo.

“Dhamira yetu ni kujenga uchumi wa watu, unaojitegemea, utakaozalisha ajira milioni 12 ndani ya miaka mitano kwa kukuza shughuli zinazoajiri watu wengi, kuongeza pato la Taifa, pato la mtu mmojammoja  na thamani ya bidhaa.”

Mbinu watakayotumia ni kuzalisha ajira mpya milioni 2.8 zitakazotokana na viwanda na itaimarisha ubora na kutafuta soko la nje kwa kazi za ubunifu kama uhunzi, uchongaji, uchoraji na bidhaa zingine zitokanazo na kazi za mikono.

“ACT Wazalendo itatengeneza ajira zenye staha zisizopungua 500,000 kwenye soko la sanaa, michezo na utamaduni kwa kuweka mifumo mizuri ya kisera na uwekezaji.”

 “Itaondoa mfumo wa zabuni katika taasisi za umma, kwenye huduma za ulinzi, usafi, ukarabati wa vifaa na majengo ili kuziongezea uwezo taasisi hizo kutoa ajira rasmi na zenye staha kwa watu wengi.” 

Itaajiri wahitimu wote wa kada za ualimu, afya na kilimo na kuweka utaratibu wa kuajiri kila mwaka wahitimu wa sekta hizo na kuimarisha uwezo wa mashirika ya umma na taasisi za Serikali kujiendesha kwa tija na faida ili kuongeza ajira.

Itashirikiana na vyama vya wafanyakazi kuboresha na kusimamia masilahi ya wafanyakazi wa sekta binafsi, ya umma, kupunguza Kodi ya Mapato ya Mfanyakazi (PAYE) ili kuwaongezea wafanyakazi kipato waweze kumudu maisha, kujiwekea akiba au kuanzisha na kuendesha shughuli za uzalishaji kipato cha ziada.

Ukiacha mbinu hizo, chama hicho pia kimeahidi kutengeneza mazingira mazuri ya kisera na kisheria yatakayowezesha vyama vya wafanyakazi kuwa huru, imara na kusimamia masilahi ya wafanyakazi kwa ufanisi.

Itarejesha mfumo wa ukokotoaji wa mafao unaomnufaisha mstaafu kulipwa kwa mkupuo asilimia 50 na Italipa malimbikizo yote ya madeni stahiki ndani ya kipindi cha miaka miwili, baada ya kuingia madarakani Oktoba 2025.

Dk Kaale alisema ahadi za kuzalisha ajira milioni nane au 12 ni kubwa na zinatekelezeka tu endapo kutakuwa na mazingira wezeshi ya kiuchumi, uwekezaji mkubwa kwenye sekta zenye uwezo wa kuajiri wengi kama kilimo, viwanda na ujasiriamali, pamoja na kuboresha elimu ya ufundi. 

Hata hivyo, alisema changamoto kama maendeleo ya sayansi na teknolojia hasa matumizi ya dijitali na akili unde, yanaweza kupunguza baadhi ya nafasi za ajira, hasa kwa kazi ambazo zinaweza kufanywa kwa urahisi kidijitali.

“Ripoti ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) ya mwaka 2023 inaonyesha vijana wengi barani Afrika, ikiwemo Tanzania, wanakabiliwa na changamoto ya kupata ajira rasmi. Ajira nyingi zilizopo zikiwa zisizo rasmi na zenye kipato kidogo,”alisema.

“Ripoti hiyo pia inasisitiza umuhimu wa kuwekeza kwenye ujuzi wa karne ya 21 na kukuza mazingira wezeshi ya ujasiriamali ili kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia,”anasema mwanazuoni huyo wa SAUT na kuongeza kuwa;

 “Bila mikakati madhubuti na ufuatiliaji wa karibu, malengo haya ni magumu kutimia,”alisema Dk Kaale ambaye pia ni mwandishi wa habari kitaaluma. 

Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Glorious Shoo alisema ajira haziwezi kutenganishwa na hali ya kisiasa, uhuru, demokrasia na amani ya kweli inayotokana na mfumo wa haki.

“Uwekezaji wa ndani na nje, ambao ndio chanzo kikuu cha ajira endelevu huwepo pale ambapo kuna uhakika wa haki, uhuru wa kutoa maoni, uwajibikaji wa viongozi, na taasisi imara kama Bunge huru linaloisimamia Serikali ipasavyo.”

“Ahadi za ajira milioni nane au 12 ni nzuri, lakini utekelezaji wake hautegemei tu mipango ya namba bali mazingira huru ya kisheria, kisiasa na kiuchumi. kabla ya kuhesabu ajira za baadaye, lazima tuanze na mabadiliko ya msingi,”alisema.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Conrad Kabewa alisema Idadi ya ajira milioni 12 kwa muda wa miaka mitano inawezekana ila kinachopaswa kuhojiwa hapo ni njia zitakazotumika kuhakikisha hizo ajira zinapatikana.

“Kutaja idadi tu haitoshi tunatakiwa kuoneshwa mikakati ya kiuchumi itakayotufikisha hapo. Kwa mfano sasaivi tuna idadi kubwa sana ya vijana waliojiajiri katika sekta isiyo rasmi – wamachinga, waendesha bodaboda n.k. Kiongozi hapaswi kujivunia uzalishaji wa aina hii ya ajira.”

“Kimsingi tumeshakubaliana kama Taifa kwamba sasa tunajenga uchumi wa soko, hatuko kwenye ujamaa tena. Sekta binafsi tunasema ndiyo injini  ya ukuaji. Sasa Serikali au sekta ya umma inafanya nini kuikuza hii sekta muhimu,”alisema na kuhoji.

“Ukizungumza na watu walio wengi serikalini wanaamini kwamba hii huwa inakua yenyewe haihitaji nguvu ya Serikali. Hapo ndipo penye shida. Viongozi wanaahidi kuongeza ajira halafu wanataka sekta inayoajiri zaidi ikue yenyewe.”

“Miaka kadhaa iliyopita nilisoma mahali Serikali ya China iliweka lengo la kuwa na mabilionea milioni 20. Hii ina maana kwamba walianzia kuwajenga tangu chini huko hadi wakafikia mahali wana uhakika wa kuwapata hao mabilionea.”