Rogath Akhwari atoa ahadi nzito RT

SIKU chache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Riadha nchini (RT), mgombea wa nafasi ua Urais, Rogath Akhwari ametoa ahadi nzito kwa kusema moja ya sababu zilizomfanya awanie nafasi hiyo ni kutaka kupunguza changamoto ya kifedha inayoikumba shirikisho hilo.

Rogath, mtoto wa gwiji wa zamani wa riadha nchini John Stephen Akhwari, ni miongoni mwa wagombea wanne wanaowania urais katika uchaguzi huo, utakaofanyika Agosti 16, jijini Mwanza.

Akizungumza na Mwanaspoti, katibu huyo wa Chama cha Riadha Mkoa wa Arusha na Kocha wa Riadha wa Polisi Tanzania, alisema anataka kuleta mabadiliko ya kweli yatakayoiwezesha RT kujitegemea kifedha na kuimarisha riadha.

Alifafanua, mchezo huo umekuwa ukipungukiwa mvuto na ufanisi nchini kutokana na changamoto mbalimbali, hasa ukata wa rasilimali fedha.

“Fedha ni changamoto kubwa RT, nitahakikisha natafuta wadhamini wa moja kwa moja ambao watatuunga mkono ili tuweze kushiriki mashindano ya kimataifa kwa ufanisi mkubwa,” alisema Akhwari.

Akhwari amelitilia mkazo kuanzisha programu ya kuendeleza vipaji vya watoto na vijana kuanzia Shule za Msingi, Sekondari hadi Taifa.

“Leo tukisema tutafute timu ya taifa ya vijana ni mtihani mkubwa, tunahitaji mfumo unaojenga vipaji endelevu,” aliongeza.

Pia alisisitiza kuijenga RT yenye misingi imara ya kiutawala, kikanuni na kisheria kwani kwa sasa shirikisho ilo halina meno na kuweka wazi atahakikisha mashindano ya taifa yanafanyika kila mkoa, hasa katika mikoa ambayo iko nyuma.

Katika historia yake michezo aliwahi kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya dunia ikiwemo Ubelgiji (2004), Ufaransa (2005), nusu marathoni ya dunia India (2004), mbio za Nyika Hispania (2000), mashindano ya Afrika Ethiopia (2007) na SADC Afrika Kusini (2007 na alishinda medali mbili za dhahabu.

Alitumika kama nahodha wa timu ya taifa ya riadha kuanzia 2001 hadi 2006 na kiufundi ana sifa za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Diploma ya ukocha wa kimataifa na mafunzo ya misuli na viungo katika michezo kutoka Chuo Kikuu cha Semmelweis, Hungary.

Diploma za uongozi wa michezo kutoka vyuo vikuu vya Leipzig na Humberg, Ujerumani, pamoja na Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino.