Unguja. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), imesema itahakikisha inaendesha uchaguzi huru wa haki bila upendeleo huku ikisisitiza kura ya mapema itakuwa palepale kama sheria ya uchaguzi inavyosema.
Kwa mujibu wa sheria namba nne ya uchaguzi ya mwaka 2018, inaeleza Zanzibar kutakuwapo na kura ya mapema na Tume imetoa kanuni inayoeleza itapigwa kabla ya uchaguzi mkuu.
Kura hiyo inawatambua watendaji wote wanaoshughulika, walinzi na wanaosimamia uchaguzi ambao wamepewa haki yao ili kutimiza majukumu yao bila changamoto zozote.
Kauli hiyo inakuja kukiwa na madai ya Chama cha ACT Wazalendo katika mikutano yake mbalimbali kudai kwamba hakitakuwa tayari kuona kura ya mapema ikiendeshwa katika uchaguzi huu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Hata hivi karibuni akiwa kisiwani Pemba, Mwenyekii wa Chama hicho, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud alirejea kauli hiyo kwamba hawatakubali kura ya mapema kupigwa Zanzibar.
Akizungumza leo Agosti 12, 2025 baada ya kufunguliwa mafunzo ya wasimamizi wasaidia wa majimbo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo, Thabit Idarous Faina amesema sheria bado ni ileile haijabadilishwa na ndio itakayotumika katika uchaguzi mwaka huu.
“Sheria ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inaeleza wazi kutakuwepo na upigaji wa kura ya mapema na ZEC imetoa kanuni inayoeleza kuwa kura ya mapema itapigwa siku moja kabla ya uchaguzi,” amesema.
Hata hivyo, amesema tume itatoa ratiba kamili ya uchaguzi Agosti 18, 2025 jinsi utakavyokuwa; “Lakini mpaka sasa sheria bado ni ileile haijabadilishwa na ndio tutakayoitumia.”
Awali, akifungua mafunzo hayo ya siku tano, Makamu Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Aziza Iddi Suweid amesema Tume inatarajia kuendesha uchaguzi huru na haki na kuhakikisha wadau wote wanaridhika.
Amesema uchaguzi mkuu ni tukio la kitaifa linalogusa maisha ya kila mwananchi, hivyo maandalizi ya uchaguzi huo ni lazima yafanywe kwa umakini, weledi, na kwa kuzingatia misingi ya haki, uwazi na uwajibikaji.
Jaji Aziza, amesema ufanisi wa uchaguzi unaanzia na uadilifu wa wasimamizi katika ngazi zote kwani hali hiyo ndio itakayoleta matokeo chanya kwenye mchakato wa uchaguzi.
“Mafanikio ya uchaguzi huu yanategemea sana utendaji kazi wenu kwani maeneo yote ya uchaguzi yanapaswa kusimamiwa kwa mujibu wa sheria, bila upendeleo wa aina yoyote kwani tunataka kuona uchaguzi unafanyika kwa uwazi, haki na kuzingatia misingi ya sheria,” amebainisha.
Kwa mujibu wa Jaji Aziza, wasimamizi wa majimbo ni kiungo muhimu katika kuhakikisha kila mpigakura anapata haki yake ya kidemokrasia hivyo ni vyema kutumia lugha nzuri wanapohudumia watu.
Amesema wanatakiwa wajue kwamba wao ndio wenye jukumu hilo kubwa la kubeba dhamana katika mchakato mzima wa uchaguzi, kwa sababu ndio watakuwa wawakilishi wa Tume kwenye majimbo watakayoyasimamia na watakaoongoza shughuli zote za maandalizi, utekelezaji na ufuatiliaji wa uchaguzi katika ngazi hiyo.
Hata hivyo, amesema ni imani yake kuwa wataongozwa na maelekezo ya sheria, kanuni za uchaguzi na miongozo iliyotolewa na Tume kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli hiyo.
Hivyo aliwasisitiza kufanya rejea katika sheria, kanuni, sera, miongozo na maelekezo yanayosimamia uchaguzi, kwani hivyo ni vitendea kazi muhimu kwao ambavyo vinapaswa kueleweka kikamilifu.
Aliwakumbusha kuwa uchaguzi si kazi ya mtu mmojammoja bali ni juhudi za pamoja kati yao, ZEC vyombo vya ulinzi na usalama, wadau wa kisiasa, asasi za kiraia, viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla.
Hivyo, “lazima kushirikiana kwa karibu na wadau hao kwa njia ya mawasiliano ya wazi na uwajibikaji.”
Mafunzo hayo ya yaliyojumuisha wasaidizi 100 yana dhamira kuu ya kuwaweka watendaji hao katika hali ya utayari kufanya shughuli za uchaguzi.
Katika siku hizo tano watafundishwa mada 15 ikiwa ni pamoja na sheria ya uchaguzi, kanuni na miongozo inayotolewa na ZEC na wao watatoa mafunzo kwa watendaji wa chini wa vituo vyote vitakavyotangazwa na Tume. Lengo ni kuhakikisha wanahitimisha jukumu zima la kuhesabu kura na kutangaza matokeo kwa ngazi ya majimbo wakati utakapofika.