Mahakama yaridhia mashahidi kesi nyingine ya Lissu kutokuonekana

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo, Dar es Salaam imeridhia mashahidi wa Jamhuri katika kesi nyingine ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ambao ni raia kutoa ushahidi bila kuonekana.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo uliotolewa leo, Jumanne, Agosti 12, 2025 na Jaji Elizabeth Mkwizu, baada ya kutupilia mbali shauri la maombi ya Lissu ya kupinga uamuzi huo uliotolewa awali na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu.

Katika uamuzi huo uliosomwa na Naibu Msajili, Livin Lyakinana, Jaji Mkwizu amesema kuwa shauri hilo halikuwa na mashiko, huku akibainisha kuwa uamuzi wa Mahakama ya Kisutu ulizingatia haki ya pande zote, mshtakiwa kusikilizwa kwa usawa na usalama wa mashahidi.

“Kuzingatia hayo yaliyoelezwa hapo juu, shauri hili linakataliwa”, amesema Lyakinana akimnukuu Jaji Mkwizu.

‎Lissu anakabiliwa na kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo katika mtandao wa Youtube, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, katika Mahakama ya Kisutu, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.

Kabla ya kuanza kwa usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka, Jamhuri (Serikali) ilifungua shauri dogo la maombi ya ulinzi wa mashahidi wake ambao ni raia (wasio askari Polisi).

Katika shauri hilo, Jamhuri iliomba mashahidi hao watoe ushahidi wao kwa kificho yaani bila kuonekana mahakamani, wala majina yao na  taarifa zao zinazoweka kufanya wakatambulika, wao binafsi, familia zao na mahali wanakoweza kupatikana.

Jamhuri ilifungua shauri hilo kwa madai kuwa mashahidi hao wamekuwa walipata vitisho kutoka kwa watu wa karibu na mshtakiwa huyo, ili wasiende Mahakama kutoa ushahidi.

Taarifa hizo zilielezwa pia katika viapo vilivyounga mkono maombi hayo, kiapo cha Wakili wa Serikali Tawabu Issa na cha Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu, Dar es Salaam (ZCO) Kamishna wa Msaidizi wa Polisi (ACP), Fsustine Mafwele.

Shauri hilo lilisikilizwa upande mmoja wa Jamhuri, kama Sheria inavyoelekeza na Hakimu Mhini katika uamuzi wake alioutoa  ‎Juni 9, 2025, alikubaliana na hoja na maombi hayo ya Jamhuri, akatoa amri hizo kama zilivyoombwa na Jamhuri.

Lissu hakukubaliana na uamuzi huo, hivyo Juni 25, 2025,  alifungua Mahakama Kuu shauri hilo la maombi ya  mapitio ya Mahakama, akiiomba mahakama hiyo iitishe jalada la kesi yake kuchunguza mwenendo na uamuzi huo kujiridhisha na uhalali na usahihi wake.

Kisha aliiomba mahakama hiyo itengue uamuzi huo wa mahakama ya chini ili mashahisi hao watoe ushahidi wao katika hali ya kawaida, yaani wafike mahakamani na kutoa ushahidi wao hadharani, wakionekana.

Shauri hilo  lilisikilizwa na Jaji Mkwizu, Julai 16, 2025, ambapo Lissu kupitia jopo la mawakili wake alibainisha na kufafanua kwa kina sababu kupinga uamuzi huo, huku jopo la mawakili wa Serikali likiziponga kwa madai kuwa hazina mashiko.

Pamoja na mambo mengine jopo la mawakili wa Lissu lilidai kuwa hapakuwa na sababu za msingi zilizotolewa kuifanya Mahakama ya chini kutoa uamuzi huo.

Mmoja wa mawakili wa Lissu, Dk Rugemeleza Nshala alidai kuwa  viapo vya hao mashahidi ambao walidai kuwa walitishiwa vilipaswa viwepo ili Hakimu aweze kutoa uamuzi wa haki, lakini hakuna viapo  walivyoviwasilisha mahakamani kama ushahidi wa madai hayo.

Wakili Jebra ‎Kambole alidai kuwa katika uamuzi ule hakimu hakufanya uchambuzi wa kiwango cha upande wa mashtaka kuthibitisha madai yao kwa kiwango kinachotakiwa, yaani bila kuacha mashaka na kwamba angefanya uchambuzi sawasawa asingeamua hivyo.

Alidai kuwa  uamuzi huo uliathiri  haki za mshtakiwa za usikilizwaji sawa, kwani Mahakama haipati fursa ya kumtathimini shahidi kuaminika kwake wakati akitoa ushahidi kizimbani wala mshtakiwa kupata fursa ya kumkabili ana kwa ana.

Kwa upande wake Wakili Jeremiah ‎Mtobesya alidai kuwa sababu zilizotolewa haziwezi kuondoa umuhimu wa Mahakama kuangalia mwenendo wa nje wa shahidi wakati akitoa ushahidi kizimbani ( demeanor).

Akijibu hoja hizo Kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali, Wakili wa Serikali Kuu, Nassoro  Katuga, kwanza alihoji iwapo  kifungu 372 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kilichotumika kufungua shauri hilo  kinaipa mahakama hiyo mamlaka kulisikiliza.

‎Alifafanua kuwa uamuzi  wa Mahakama ya Kisutu  unaolalamikiwa , ulitolewa kwa mujibu wa sheria na kwamba Mahakama ilijikita katika ushahidi wa viapo viwili vilivyotolewa  Wakili wa Serikali ZCO, ACP  Mafwele.

‎Wakili Katuga alidai kuwa kiapo cha ACP Mafwele, kilieleza kuwa amepokea taarifa fiche kuwa kuna mashahidi ambao sio polisi kuwa wamekuwa wakipokea vitisho vya kutoa ushahidi katika kesi hizo.

Jaji Mkwizu katika uamuzi wake leo, kama ulivyosomwa na Naibu Msajili Lyakinana ametupilia mbali hoja za Lissu akisema kuwa madai yake hayana mashiko kisheria.

Kuhusu hoja ya viapo vya mashahidi hao wanaodai kutishiwa  kutokuambatanishwa katika shauri la maombi ya Jamhuri, amesema kuwa Mwenendo inaonesha kuwa kulikuwa na viapo vya Wakili wa Serikali na ACP Mafwele.

Jaji Mkwizu amesema kuwa si takwa la kisheria mashahidi hao kuwasilisha mahakamani viapo vyao.

Pia, Jaji Mkwizu ametupilia mbali hoja za mawakili wa Lissu kuwa hata hicho kiapo cha ACP Mafwele hakikuwa na taarifa na maelezo ya kutosha ya hao mashahidi wanaodai kutishiwa na kwamba zilikuwa ni taarifa za kusikia.

Jaji Mkwizu amesema kuwa kwanza kuwepo kwa taarifa hizo kwenye kiapo hicho  kungeweza kufanya wajulikane na hivyo kuathiri usalama wao, huku akisisitiza kuwa pia si takwa la kisheria kwa taarifa hizo kuwekwa kwenye kiapo hicho.

Jaji Mkwizu amesema kuwa taarifa za ACP Mafwele si za kusikia Baki ni taarifa rasmi kwa kuwa ni ofisa wa Serikali mwenye dhamana ya kuchinguza tuhuma za uhalifu.

Amesema kuwa uamuzi wa Hakimu ulizingatia haki ya kusikilizwa ya mshtakiwa kwani Mahakama bado ina mamlaka ya kutathimini mwonekano wa nje wa shahidi anapotoa ushahidi unaweza kuathiri tathimini (demeanor).

Awali Jaji Mkwizu ametoa uamuzi wa malalamiko aliyoyatoaLissu ya kuzuiwa na askari Magereza kuwasiliana na mawakili wake na kubadilishana nyaraka mbalimbali.

Katika uamuzi huo pamoja na mambo mengine Jaji Mkwizu amesema kuwa usiri wa mawasiliano kati ya wakili na mteja wake ni na kupeana nyaraka za mbalimbali haki ya msingi.

Hivyo ameelekeza mshtakiwa asizuiwe kuwasiliana na mawakili na kupewa nyaraka bila sababu za msingi.

Hata hivyo, Jaji Mkwizu amesema  kuwa haki hiyo ina mipaka kwa ajili ya usalama wa gereza na wafungwa.

Amesisitiza kuwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Jeshi la Magereza, askari magereza wana wajibu wa ulinzi na usalama wa wafungwa/mahabusu ndani na nje ya gereza.

Mbali na kesi hii pia Lissu anakabiliwa na kesi nyingine ya uhaini, ambayo pia Mahakama Kuu imesharidhia maombi ya Jamhuri mashahidi wake kutoa ushahidi wao kifichoni, majina yao na taarifa zinazoweza kuwafanya wakatambulika kutokuwekwa wazi.

‎Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu. Katika mashtaka hayo Lissu anadaiwa kumhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutenguliwa kwa wagombea chama chake katika maeneo mbalimbali wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, 2024.

‎Pia anadaiwa kuwatuhumu askari Polisi kuhusika katika wizi wa kura kupitia vibegi na majaji kutokutenda haki kwa madai ya kutaka wapate uteuzi wa Rais kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani.

‎Anadaiwa kutenda makosa hayo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai umma.