Farida Mangube, Morogoro
KATIKA kuendeleza kilimo na ufugaji wenye tija, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendelea kuwa mshirika muhimu wa wakulima na wafugaji nchini kupitia tafiti zake za kisayansi zinazolenga uzalishaji wa malisho bora kwa mifugo.
Katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yaliofanyika mkoani Morogoro, banda la SUA limevutia mamia ya wakulima, wafugaji na viongozi waliokuja kujifunza mbinu za kisasa za kuzalisha na kuhifadhi malisho.
Wataalamu wa SUA wamesema changamoto kubwa kwa wafugaji nchini ni uhaba wa malisho hasa nyakati za kiangazi, hali inayosababisha mifugo kudhoofika na mara nyingine kupelekea migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Ahmed Amasha ni Afisa mifugo kutoka Chuo kikuu SUA, anasema matumizi ya mbegu bora za nyasi na mikunde ya malisho, pamoja na mbinu za uvunaji na uhifadhi wa malisho (haymaking na silage), vinaweza kuongeza uzalishaji wa chakula cha mifugo kwa zaidi ya mara mbili katika eneo lilelile.
“Mbegu hizi siyo tu zinastahimili ukame, bali pia zina virutubisho vya kutosha vinavyohitajika kwa mifugo ili kutoa mazao ya nyama na maziwa yenye ubora,” amesema Amasha, Ameongeza kuwa mfumo wa kulishia mifugo kwa zamu kwenye sehemu zilizopangwa (rotational grazing) husaidia kudumisha uzalishaji wa malisho mwaka mzima bila kuharibu ardhi.
Akizungumza baada ya kutembelea banda la SUA, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Ndemanga, amepongeza chuo hicho kwa mchango wake mkubwa kwa jamii. “Tukiwa viongozi ambao pia ni wakulima na wafugaji, tumeshuhudia namna SUA inavyotoa elimu ya vitendo kuhusu uzalishaji na uendelezaji wa malisho bora. Hii ni elimu muhimu sana kwa wafugaji wa sasa,” amesema Mhe. Ndemanga.
Amebainisha kuwa iwapo wafugaji watatumia mbegu bora na mbinu za kisayansi zinazofundishwa na SUA, wataweza kuepukana na mfumo wa kuhamahama kutafuta malisho na badala yake kutumia maeneo madogo kuzalisha chakula cha kutosha kwa mifugo. “Kwa mfano, ekari moja ya ardhi inaweza kugawanywa katika sehemu nne na kutumika kwa zamu kulishia mifugo, huku kila sehemu ikipumzishwa na kumwagiliwa baada ya matumizi ili kurejesha hali yake ya awali,” amesema Mkuu wa Wilaya.
Kupitia utafiti, mafunzo ya kitaalamu na usambazaji wa mbegu bora, SUA inaendeleza dhamira yake ya kusaidia wakulima na wafugaji kuboresha maisha yao na kupunguza migogoro ya mara kwa mara kati ya makundi hayo.