Mnigeria akoshwa  viwango vya wenyeji  CHAN 2024, akizitaja Simba na Yanga 

MWANDISHI wa Habari kutoka Nigeria, Samweli Areo, aliyepo Zanzibar kwa sasa, amepongeza maendeleo makubwa ya soka la Afrika Mashariki, akisema kiwango cha timu za taifa za ukanda huo kimeimarika na kuleta ushindani wa kweli katika mashindano ya CHAN 2024.

Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi Digital,  Areo amesema ubora wa klabu za  Simba na Yanga umechochea kuifanya Taifa Stars kuweka historia katika michuano hiyo.

“Sikuwahi kutarajia makubwa kutoka Kenya, kwa kuwa ni michuano yao ya kwanza, lakini kocha Benny McCarthy, ameleta mabadiliko makubwa katika fikra za wachezaji. Mashabiki pia wameunga mkono kikosi chao ipasavyo,” amesema Areo.

Kenya imewashangaza wengi katika Kundi A kwa kumfunga bingwa mara mbili wa michuano ya CHAN, Morocco na kufikisha pointi saba kileleni, huku ikisaliwa na mechi moja dhidi ya Zambia.

Aliongeza, Uganda pia imepiga hatua kubwa na kufanya vizuri, hali iliyomfanya kabla ya mashindano kuwapa nafasi kubwa zaidi Tanzania kutokana na maandalizi yake.

“Baada ya Tanzania kushinda mashindano ya maandalizi ya  CECAFA dhidi ya Senegal na Uganda, niliona wako tayari kushindana. Sishangai kuona wamefanikiwa kushinda mechi tatu na kukusanya alama za kutosha na kuingia robo fainali. Kwa msaada wa mashabiki, wanaweza kufika mbali,” amesema.

Taifa Stars imekusanya pointi tisa kupitia mechi tatu kwa kuzifunga, Burkina Faso kwa mabao 2-0, Mauritania bao 1-0 na Madagascar kwa mabao 2-1.

Uganda ikiwa Kundi C, ilianza vibaya kwa kuchapwa 3-0 na Algeria, lakini ilizinduka na kuzifunga Guinea na Niger hivyo inaongoza kundi ikiwa na pointi sita. 

Kwa Areo, mafanikio haya ya pamoja yanaongeza mvuto wa mashindano na kuongeza idadi ya watazamaji viwanjani, jambo linaloinufaisha Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Hata hivyo, mwandishi huyo alisema muda wa mashindano hayo, ungekuwa bora zaidi kama yangefanyika Februari kama ilivyopangwa awali.