KUNA taarifa za uhakika kutoka kwa uongozi wa Namungo kuwa umerejesha majeshi kwa kocha Juma Mgunda, ambaye ilidaiwa wameachana naye pamoja na msaidizi wake Shadrack Nsajigwa, lakini baada ya kufanya tathimini wameona bado anawafaa.
Chanzo cha ndani kutoka Namungo, kilisema kuna asilimia kubwa ya kuendelea na Mgunda msimu ujao ambapo atakuwa anasaidiana na Ngawina Ngawina, hivyo kumchukua kocha Aman Josiah ali-yekuwa Tanzania Prisons, huenda likawa gumu kwa sasa.
“Ni kweli tulitaka kuachana na Mgunda na kumchukua Josiah aliyeisaidia Tanzania Prisons kusalia Ligi Kuu msimu uliyopita, kutokana na vikao vya tathmini tunavyofanya mara kwa mara, tukaona Mgunda ana uzoefu mkubwa,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Kwa sasa Mgunda yupo timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayoshiriki michuano ya Chan, hivyo tunatarajia (kesho) leo kwenda kuweka kambi Dodoma timu kwa muda huo itakuwa chini ya Ngawina.
“Timu itakaa Dodoma wiki tatu ambapo tutacheza mechi mbalimbali za kirafiki, viwanja ambavyo tutakuwa tunavitumia kwa mazoezi Utumishi.”
Chanzo hicho kilisema mshambuliaji wa kimataifa, Heritier Makambo waliyemsajili kutoka Tabora Unit-ed ambako alimaliza na mabao sita na asisti nne anatarajia kuingia nchini Ijumaa ya wiki hii.
“Kuhusu kumsajili kwa mkopo kipa Ally Salim kutoka Simba hilo linashindikana, ila tutakuwa na beki Hussein Kazi ambaye tulimchukua kama mchezaji huru kutoka klabu hiyo,” kilisema chanzo hicho.