SIMBA Queens inaendelea kushusha nyota wa kimataifa na wale wa ndani, lakini inaelezwa imemuongezea mkataba wa mwaka mmoja winga wa timu hiyo, Elizabeth Wambui.
Msimu uliopita Mkenya huyo alimaliza na mabao saba na asisti tatu kwenye mechi 16 alizocheza, nyuma ya Asha Djafar aliyefunga manane na Jentrix Shikangwa aliyeweka kambani mabao 24.
Mmoja wa watu wa karibu wa mchezaji huyo aliliambia Mwanaspoti kwamba Simba ilimuwekea ofa nono ya kumshawishi asalie kikosini hapo baada ya kuonyesha kiwango kikubwa msimu uliopita.
Aliongeza kuwa mbali na Simba kulikuwa na ofa nyingine kutoka Besiktas ya Uturuki, lakini lilishindikana kutokana na kutoelewana baadhi ya mambo baina ya upande wa mchezaji na timu.
“Kulikuwa na changamoto kwenye ofa ya Uturuki, mambo yalikuwa mengi lakini mchezaji akaamua kubaki Simba baada ya kumuwekea ofa nzuri na uhakika wa nafasi yake kwenye kikosi hicho,” alisema mtu huyo na kuongeza:
“Ni mchezaji mzuri ambaye alitupa kila kitu msimu uliopita, kasi, nguvu na akili ya kuwapita mabeki vimewashawishi kumbakisha na tayari amesaini, ila kwa sasa yuko kwao Kenya.”
Kwa wachezaji waliocheza msimu uliopita wakaongezewa mikataba ni pamoja na Wambui, Shikangwa, kiungo Vivian Corazone ambaye bado ana mkataba, Wilfrida Cedar na Ruth Ingosi.